Akizungumzakwenye mji mkuu Beirut, wakati wa ziara aliyoiita ya mshikamano na wananchi wa taifa hilo la Mashariki ya Kati, Guterres amesema kwamba maneno ya kuunga mkono lazima yaambatane na hatua za vitendo.

Ombi hili ni kufanikisha usaidizi kwa miezi mitatu

“Wito huu mpya unalenga kuongeza misaada ya kuokoa maisha katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, ikijumuisha chakula, maji safi, huduma za afya, elimu, huduma za ulinzi, na misaada mingine muhimu,” amesema Guterres kwenye hotuba yake.

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa ongezeko la mapigano ya kijeshi katika eneo hilo linaathiri kwa kiasi kikubwa Lebanon.

“Amebainisha kuwa mamia ya raia wameuawa, wakiwemo watoto, huku jamii nzima zikiwa zimeyahama makazi yao. Zaidi ya watu 816,000 wamehama ndani ya nchi, na zaidi ya watu 90,000—wengi wao wasyria lakini pia walebanoni wamekimbilia nchini Syria.

Guterres amesisitiza kuwa upatikanaji wa huduma za msingi kama chakula, maji, huduma za afya, na elimu umevurugika kwa kiwango kikubwa, huku amri za kuhamisha watu zikienea katika maeneo mapya zaidi ya nchi kuliko hapo awali.

Heko watumishi mnaoendelea kujitolea

Licha ya changamoto hizo, amepongeza ustahimilivu wa jamii za wenyeji, shule zinazohifadhi familia zilizohamishwa, na wahudumu wa afya wanaoendelea kufanya kazi chini ya shinikizo kubwa.

“Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wa misaada ya kibinadamu wanafanya kazi kwa karibu na mamlaka za kitaifa kutoa msaada wa dharura, ikiwemo chakula cha moto na vifaa muhimu.” Amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa mafanikio ya ombi hilo la dharura  yanategemea ufadhili wa haraka na unaonyumbulika, pamoja na usalama ili wahudumu wa misaada ya kibinadamu wawafikie wenye uhitaji.

Akihitimisha kauli zake, Guterres amesema wakati huu taifa hilo lina changamoto na mahitaji makubwa, huu ni wakati wa jumuiya ya kimataifa kuonesha mshikamano wake kwa kufanikisha ombi hilo la dharura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *