Dar es Salaam. Tofauti  na ulivyo ukubwa wa jina lake ndani ya Bongofleva, mwimbaji Ommy Dimpoz, 38, ni kama ameamua kuupa kisogo muziki ambao ndio hasa uliompatia umaarufu alionao kwa wakati huu.

Ommy Dimpoz, mkali wa kibao cha Me and You (2013), sasa ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu bila kutoa wimbo wowote kwa ajili ya mashabiki wake, kitu ambacho sio kawaida kwa msanii mkubwa kama yeye.

Wimbo wake mwisho kuachia ulitoka Septemba 2024, na tangu wakati huo amekuwa kimya. Wimbo huo unakwenda kwa jina la ‘Nitakupa’ akiwa amemshirikisha Jay Melody, staa aliyekulia Tanzania House Talent (THT).

Mradi huo ulikuja baada ya kimya kingine kirefu tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, Dedication (2022) chini ya Sony Music na RockStar Africa, huku ikiwa na nyimbo 15 pamoja na kuwashirikisha wasanii 10 kutoka Bongo na kimataifa.

Utakumbuka kuwa Ommy Dimpoz alianza safari ya muziki akiwa sekondari katika kundi lao walilolipa jina la VIP lililoundwa na watu wanne, kisha akaja kujiunga na Top Band yake TID akiungana na waimbaji wengine akiwemo Steve RnB.

Hatimaye alitoka kimuziki kupitia kibao chake, Nai Nai (2012) kilichotayarishwa na KTG. Kufanya vizuri kwa wimbo huo kulimwezesha kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi akipokea kijiti hicho kutoka kwa Linah aliyeshinda msimu wa 2011.

Anashikilia rekodi kama msanii pekee Bongo kushinda TMA mara mbili mfululizo katika kipengele cha Wimbo Bora wa kushirikiana akishinda 2012 na 2013 kupitia ngoma zake ‘Nai Nai’ na ‘Me and You’ alizoshirikiana na Alikiba, na Vanessa Mdee.

Mbali na TMA, Ommy Dimpoz ameshinda tuzo nyingine kama African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA), ameanzisha lebo yake, Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, na sasa anafanya kazi na RockStar Africa pamoja na  Sony Music Entertainment Africa.

Hata hivyo, baada ya mafanikio makubwa ya hapa na pale, ni kama Ommy Dimpoz hana tena ile njaa ya kupiga hatua kubwa kimuziki ambayo alikuwa nayo miaka 14 iliyopita.

Kwa sasa kutoa wimbo mmoja baada ya miaka miwili sio shida zake, ndivyo mambo yake yanavyoenda.

Lakini kwa namna mtindo wake wa maisha unavyoonekana kila mara katika mitandao ya kijamii, sio kwamba hawezi kufanya hivyo, pengine ndio utararibu aliojiwekea au aliowekewa na lebo au menejimenti inayosimamia muziki wake wakati huu.

Lakini, Ommy Dimpoz sio msanii wa kwanza kufanya hivyo, wapo wengi tu hapa Bongo walishakaa kimya muda mrefu na baadaye wakarejea kwa kishindo, mathalani ni ujio mpya wa Alikiba kupitia wimbo wake, Mwana (2014) baada ya kupumzika muziki kutokana na kile alichodai ni ili kuwa karibu na familia yake.

Hata hivyo, kwa Ommy Dimpoz ipo tofauti maana vipindi kama hivyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara, jambo linalofanya muziki wake kutozungumziwa kwa ukubwa wake au mashabiki kutomzingatia vya kutosha pale anapotoa kazi mpya.

Ikumbukwe hata albamu yake ilitoka kwa kuchelewa sana, yaani ilikuja miaka 10 baada ya yeye kutoka kimuziki wakati wasanii wengi hutoa albamu ndani ya miaka mitatu hadi mitano ya mwanzo ya umaarufu wao katika tasnia.

Na katika nyimbo 15 za albamu yake hiyo, Dedication (2022), ni mbili pekee ambazo zilitolewa video zake, nyimbo hizo ni ‘Vacation’ uliotoka kabla ya albamu hiyo, na mwingine ni ‘Anaconda’ akilishirikisha kundi la Black Diamond kutokea Afrika Kusini, ambalo lilifanya kazi na Alikiba hapo awali.

Kwa Bongo, mashabiki wengi walitegemea kolabo yake na Fally Ipupa ‘Mom Bebe’ kutoka ndani ya albamu hiyo ingefanyiwa video kali lakini hajawa hivyo hadi sasa licha ya ukubwa wa gwiji hiyo kutoka DR Congo aliyeshirikiana na Diamond Platnumz hapo awali pia.

Ommy Dimpoz katika moja ya mahojiano yake, alisema alikutana na Fally Ipupa huko Mwanza na wakakubaliana warekodi, lakini Fally akamwambia inabidi amfuate Paris, Ufaransa ambapo ndipo walirekodi na Dimpoz hakumlipa fedha kwa kufanya kolabo hiyo ila ndio hivyo video haijapatikana hadi leo. Kulingana na taarifa ambazo ziliwahi kuwekwa katika akaunti yake ya Boomplay Music, utajiri wake unakadiriwa kuwa ni Dola2 milioni (wastani wa Sh5 bilioni), hivyo kwa upande mwingine unaweza kusema kunyata kwake kimuziki kunaweza kusitokane na changamoto za kiuchumi.

Ikumbukwe baada ya kuimba vizuri wimbo wa Mr Paul, Zuwena, ndipo TID akakubali kumjumuisha Ommy Dimpoz ndani ya Top Band, na tangu hapo akaanza kupanda ngazi kimuziki hadi alipokuja kuwa mwimbaji mkubwa wa Bongofleva.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *