
Musoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) Mkoa wa Mara imefanikisha malipo ya Sh4.2 milioni kwa mwalimu wa shule ya msingi wilayani Tarime, fedha za uhamisho alizokuwa akizidai kwa zaidi ya miaka minane.
Mwalimu huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Samuel Magutu, alikuwa anadai fedha hizo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime District Council baada ya kuhamishwa kutoka Shule ya Msingi Magoto kwenda Shule ya Msingi Itiryo, wilayani humo.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, mjini Musoma Machi 13, 2026, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Simon Ngoma, amesema malipo hayo yalicheleweshwa kutokana na urasimu katika mamlaka husika.
Ngoma amesema baada ya kupokea malalamiko ya mwalimu huyo, taasisi hiyo ilianza uchunguzi na kubaini kuwa hakukuwa na sababu ya msingi iliyosababisha malipo hayo kucheleweshwa kwa muda mrefu.
“Tuliagiza mwalimu alipwe na leo ninafuraha kuwajulisha kuwa tayari amelipwa. Pia tumeelekeza mamlaka husika kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi,” amesema Ngoma.
Amesema uchunguzi wa Takukuru umebaini kuwapo watumishi wengine wanaokabiliwa na changamoto kama hiyo lakini hawatoi taarifa ili zipatiwe ufumbuzi.
“Hata mwalimu Magutu ilimchukua muda mrefu sana kabla ya kuja ofisini kutoa taarifa. Nawahimiza wananchi na watumishi wote wasikae kimya na changamoto zao; wazifikishe ofisini ili zipatiwe ufumbuzi au waelekezwe mahali sahihi pa kupata msaada,” amesema.
Familia ya mwalimu mstaafu yalipwa Sh50 milioni
Katika hatua nyingine, Ngoma amesema Takukuru imefanikisha pia familia ya mwalimu mstaafu Bigambo Mashauri kulipwa Sh50 milioni zilizodaiwa kuchukuliwa kinyume cha utaratibu na mwalimu mwenzake, Fedson Mainya.
Amesema familia ya marehemu Mashauri iliwasilisha taarifa kwa Takukuru kuhusu malipo ya Sh50 milioni yaliyofanyika baada ya mwalimu huyo kustaafu, fedha ambazo zilidaiwa kuwa kwa ajili ya ununuzi wa shamba.
“Huyu mwalimu mstaafu alifariki dunia baada ya kustaafu mwaka 2020 na kulipwa mafao mwaka 2021. Nyaraka zinaonyesha kuwa siku moja baada ya kulipwa mafao walienda benki na akaidhinisha malipo hayo kwa mwalimu mwenzake bila kuwepo vielelezo vinavyoeleza sababu ya malipo hayo,” amesema Ngoma.
Amesema msimamizi wa mirathi alipofuatilia alielezwa kuwa fedha hizo zilikuwa za kununua shamba, lakini mhusika alishindwa kueleza lilipo shamba hilo, jambo lililozua shaka na kupelekea taarifa kutolewa Takukuru.
Baada ya uchunguzi kufanyika, Ngoma amesema ilibainika kuwa hakukuwa na shamba wala mkataba wa mauziano, hivyo mwalimu huyo aliamuriwa kurejesha fedha hizo, jambo alilolitekeleza.
Aidha, amesema katika kipindi hicho Takukuru ilifuatilia miradi 31 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh14.9 bilioni ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika ipasavyo.
Kwa mujibu wa Ngoma, ufuatiliaji huo ulibaini kasoro kadhaa ambazo wahusika walipewa maelekezo ya kuzifanyia kazi.
Baadhi ya watumishi ambao hawakutaka majina yao kutajwa wamesema ucheleweshaji wa malipo ya stahiki kwa watumishi ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa.
“Unaona kama huyo mwalimu kwa miaka minane yote amekuwa akihangaikia Sh4 milioni tu. Huu ni uonevu wa hali ya juu, kuna urasimu mkubwa sana. Naiomba Takukuru iendelee kumulika ofisi hizi,” amesema mmoja wa watumishi hao.
Mwalimu mwingine ameiomba Takukuru kuendelea kufuatilia madai ya aina hiyo ili watumishi wanaokabiliwa na changamoto kama hizo waweze kupata ufumbuzi kwa wakati.