Wasomi na watu mashuhuri kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wamelaani mashambulizi na jinai zinazofanywa na Marekani na Israel dhidi ya watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Muhammad Sadeq al Hashemi ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Iraq, ametuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akilaani vikali mashambulizi ya Marekani na Israel nchini Iran.

Al Hashemi amesema: Mauaji ya watoto wadogo na kushambulia miundomsingi ya kiraia kwa makusudi, zikiwemo hospitali na vituo vya afya nchini Iran, ni miongoni mwa jinai mbaya zaidi dhidi ya binadamu.

Sadeq al Hashemi amesema, jinai hizi zinadhihirisha na kuweka wazi ukatili wa maadui na jinsi wanavyopuuza maadili na thamani za kibinadamu.

Kwa upande wake, mwandishi mtajika wa Italia, Maria Morigi, amelaani vikali mashambulizi yasiyo na sababu yoyote ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kusema: “Ninatangaza mshikamano wangu na watu na serikali ya Iran katika kipindi cha kusikitisha sana cha sasa ambapo ukatili wa Kikoloni-Kizayuni wa Israel unaonekana waziwazi kwa walimwengu.”

Heba Smith, Rais wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu wa Uruguay ya Fatima Zahra (AS) pia ametuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akisema: “Hakuna shambulio lolote baya zaidi kama kushambulia watoto wadogo. Tunalaani vikali shambulizi la utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa Kibeberu wa Marekani dhidi ya Iran.”

Heba Smith ameongeza: “Tunatangaza mshikamano wetu na watu wa Iran katika kipindi hiki ambapo zinatolewa habari mpya za ukiukwaji wa haki za binadamu na mauaji ya watu wasio na hatia katika nchi hiyo.”

Wakati huo huo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Australia, Prf. Tim Anderson ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akilaani jinai za Marekani na Israel nchini Iran hasa shambulizi lililolenga Shule ya Msingi ya Shajarah Tayyiba ya wasichana kusini mwa Iran. Amesema: “Ninatangaza hasira na kuchukizwa sana na jinai za kikatili na mashambulizi ya watenda jinai wa Kimarekani-Kiisraeli dhidi ya raia wa Iran.”

Na kituo cha vyombo vya habari cha Turkish Harici Media kimetoa taarifa kikitangaza kuwa: “Tunasimama bega kwa bega na watu wa Iran katika vita hivi vya ukatili, haramu na visivyo vya haki ambavyo vinalenga viongozi wa kisiasa, wananchi wa kawaida, mahospitali, shule na vyombo vya habari.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *