
Mamilioni ya waombolezaji leo Jumatano walikusanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala nchini Iraq kwa ajili ya kuaga na kutoa heshima zao za mwisho kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na familia yake waliouliwa shahidi katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Msafara rasmi wa kumuaga Ayatullah Sayyid Ali Khamenei huko Iraq ulianza leo saa 12 asubuhi kwa saa za Iraq katika mji mtakatifu wa Najaf, baada ya Swala ya Maiti katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (AS).
Baada ya mwili wa Imam Khamenei kuswaliwa, msafara huo uliondoka katika haramu tukufu la Imam Ali (AS) na kupita katika daraja la Kufa na katika makutano ya Thawrat al-Ashreen kuelekea uwanja wa al-Sadreen, kabla ya mwili huo kuelekea Karbala.
Harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq, al Hashd al Sha’abi imeeleza kuwa mapema leo zaidi ya watu milioni 2.3 wameshiriki katika marasimu ya kumuaga hayati Imam Sayyid Ali Khamenei mjini Najaf, na kwamba idadi hiyo ilikuwa ikiendelea kuongezeka huku waombolezaji wakifika kutoka sehemu mbalimbali za Iraq.
Kituo cha televisheni cha Al Mayadeen kimeunukuu uongozi wa mamlaka ya mji wa Karbala na kuripoti kuwa maafisa husika wa mji huo wamesajili waombolezaji milioni 7.
Waombolezaji walimiminika katika mji wa Najaf kutoka maeneo mbalimbali ya Iraq, ambao umeshuhudiwa mkusanyiko mkubwa wa watu ambao haujawahi kuonekana.
Barabara zinazoelekea katika mji mtukufu wa Najaf zilikuwa na msongamano mkubwa huku waombolezaji wakisafiri kutoka mikoa mbalimbali ya Iraq ikiwemo Basra, Muthanna na Maysan.
Njia ya msafara wa kumuaga Kiongozi Shahidi yenye urefu wa kilomita sita ilijaa waombolezaji waliokuwa wamebeba picha za Ayatullah Khamenei na kupeperusha bendera za Iraq, Iran na harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.
Baada ya kufika Karbala, miili ya Imam Khamenei na familia yake ilipelekwa kwenye Haram tukufu ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali (AS) na kaka yake Abbas (AS), kwa marasimu ya heshima za mwisho na kuaga.