
Geneva, Uswisi. Msimamizi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Gina Romero, ameisifu Tanzania kwa kuunda Tume huru ya Uchunguzi kuhusu matukio yaliyotokea Oktoba mwaka jana, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya nchi katika kulinda haki za binadamu.
Romero ametoa kauli hiyo Machi 12, 2026 mjini Geneva wakati akihitimisha mjadala uliokuwa na mada ya Ukweli na Uwajibikaji katika Matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa 2025.
Amesema kuundwa kwa tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, kunaonesha utayari wa Tanzania kuzingatia haki za binadamu na kufanya uchunguzi huru kuhusu matukio hayo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, pia ameipongeza tume hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, United Nations Human Rights Council, kilichofanyika Geneva wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 12, tume hiyo imepata kuungwa mkono kutokana na rekodi ya weledi na uadilifu wa Jaji Chande, ambaye amewahi kushiriki katika uchunguzi mbalimbali wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo uchunguzi wa tuhuma za mauaji holela katika mji wa El Fasher nchini Sudan.
Aidha, Jaji Chande aliwahi kuongoza jopo la uchunguzi kuhusu ajali ya ndege iliyomuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjöld.
Wakati huo huo, taarifa hiyo imekuja katika kipindi ambacho mashirika ya Amnesty International na Human Rights Watch yamekiri kuwa baadhi ya ripoti zao kuhusu matukio ya Oktoba 29 mwaka jana zilikuwa na mwelekeo wa upande mmoja.
Awali, mashirika hayo yalidai kulikuwa na matumizi makubwa ya nguvu katika kudhibiti vurugu zilizohusiana na uchaguzi, madai ambayo Serikali ya Tanzania iliyapinga na kutoa ufafanuzi wake.
Katika kikao cha 61 cha UNHRC, serikali ilieleza msimamo wake kuhusu suala hilo na kupata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wadau, wakiwemo wawakilishi kutoka Zimbabwe, waliotilia shaka weledi na uadilifu wa mashirika hayo mawili katika kuandaa ripoti zao.
Kwa mujibu wa mjadala huo, baadhi ya washiriki walieleza kuwa ripoti za mashirika hayo zilionekana kuathiriwa na misukumo ya kisiasa badala ya kuzingatia juhudi za kutafuta ukweli kwa kutoa nafasi sawa kwa pande zote.
Katika maelezo yake, Serikali ya Tanzania ilikosoa mashirika hayo kwa kile ilichodai ni upendeleo wa kisiasa, kupuuza waliodaiwa kuanzisha na kuchochea vurugu, kushindwa kuthibitisha taarifa zao ipasavyo, pamoja na kutotambua mchango wa vyombo vya usalama katika kulinda usalama wa taifa na kudumisha utawala wa sheria.
Serikali pia ilieleza kuwa wakati wa kipindi cha uchaguzi, mitandao ya kijamii ilijaa ujumbe uliokuwa ukichochea chuki, vurugu na hata kauli zilizotafsiriwa kuwa za uhaini kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, watu binafsi na mashirika ya kiraia ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania ilihoji kwa nini matukio hayo hayakuonekana katika ripoti za Amnesty International na Human Rights Watch.
Katika wasilisho lake, serikali pia ilizitaka taasisi hizo kutoa mwongozo na mapendekezo ya wazi kuhusu kiwango cha nguvu kinachopaswa kutumika katika kulinda maisha ya watu, kudumisha utawala wa sheria na kuhifadhi mamlaka ya dola wakati wa matukio ya vurugu.