Mgogoro katika eneo la Mashariki ya Kati umeingia wiki yake ya tatu huku mapigano yakiendelea katika maeneo mbalimbali ya kanda hiyo na mahitaji ya kibinadamu yakizidi kuongezeka.
Bei ya mafuta imeendelea kubaki karibu dola 100 kwa pipa, huku usumbufu katika usafirishaji wa baharini na kufutwa kwa safari za ndege ukiathiri usafiri na minyororo ya usambazaji wa bidhaa na misaada umesema Umoja wa Mataifa.
Licha ya changamoto kubwa za usafirishaji na usalama, hata hivyo mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yanaongeza misaada ya dharura, yakionya kuwa kuongezeka kwa wakimbizi wa ndani, uhaba wa chakula na shinikizo kwa mifumo ya afya vitaongezeka kadri mgogoro unavyoenea.
Wanajeshi wa kulinda amani wa UNIFIL wakipiga doria kusini mwa Lebanon. (Maktaba)
Walinda amani wa UN washambuliwa kusini mwa Lebanon
Kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, (UNIFIL), kimeripoti kuwa doria zake zilishambuliwa kwa risasi tarehe jana 15 Machi katika matukio matatu tofauti karibu na eneo lake la operesheni kusini mwa Lebanon.
Katika tukio moja mjini Yatar, risasi zilidondoka umbali wa takribani mita tano kutoka kwa walinda amani. UNIFIL ilisema doria mbili zilijibu mashambulizi hayo kwa kujilinda kabla ya kuendelea na shughuli zao. Hakuna mwanajeshi wa kulinda amani aliyejeruhiwa katika matukio hayo.
Ujumbe huo umesisitiza kuwa uwepo wa silaha nje ya udhibiti wa serikali katika eneo lake la operesheni ni ukiukwaji wa azimio namba 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ukionya kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa hayakubaliki na yanaweza kuhesabiwa kuwa uhalifu wa kivita.
Waafghanistan wanawasili kwenye bandari ya Islam Qala kutoka Iran kwenda Afghanistan.
WFP yaongeza msaada wa chakula Afghanistan
Wakati huo huo katika eneo pana la kanda hiyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, (WFP), limesema linaongeza misaada ya dharura ya chakula nchini Afghanistan ambako migogoro na ukosefu wa utulivu wa kikanda vinaongeza zaidi janga kubwa la njaa ambalo tayari lipo
WFP inawasilisha msaada wa chakula unaookoa maisha kwa zaidi ya familia 20,000 zilizolazimika kuyahama makazi yao katika majimbo kadhaa, ikiwemo Nuristan, Kunar na Kandahar. Operesheni za misaada zinaendelea licha ya ghasia na kuvurugika kwa njia za biashara.
WFP inaonya kuwa ukosefu wa utulivu katika nchi jirani na mgogoro mpana wa Mashariki ya Kati unasukuma bei za chakula kupanda na kutishia minyororo ya usambazaji, hali inayoongeza hatari ya njaa kali zaidi katika nchi ambayo tayari mamilioni ya watu wanategemea msaada wa dharura.
Licha ya mazingira hatarishi katika maeneo hayo, WFP imeanza tena shughuli zake katika maeneo mengi ya mpakani.
Familia zilizofurushwa na mgogoro nchini Lebanon wanapokea vifaa kutoka kwa mashirika ya kibinadamu.
Msaada kwa waliokimbia makazi yao
Aidha, msaada kwa familia zilizokimbia makazi yao unatarajiwa kuwafikia watu katika majimbo manane. Operesheni hizo zinaanza mashariki mwa Afghanistan katika majimbo ya Nuristan, Kunar na Nangarhar, kisha kuelekea kusini kupitia Paktya, Khost na Paktika, na kuendelea hadi Zabul na Kandahar katika mpaka wa kusini wa Afghanistan.
“Huu ni mgogoro juu ya mgogoro: baada ya kustahimili mishtuko kama kupoteza ajira na matetemeko ya ardhi, familia ambazo tayari zilikuwa zinakabiliwa na njaa nyingi zikiwa na akina mama na watoto wenye utapiamlo sasa zinajikuta katika mstari wa mbele wa mapigano,” amesema John Aylieff. “Hatuwezi kugeuza macho yetu, Afghanistan imejikuta kati ya migogoro miwili, na ukosefu wowote wa utulivu zaidi utasukuma mamilioni ya watu zaidi katika njaa huku ukiongeza shinikizo katika kanda ambayo tayari iko ukingoni.”
Kufungwa kwa mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan tangu Oktoba mwaka jana pamoja na kuongezeka kwa mapigano Mashariki ya Kati kunaleta changamoto kubwa kwa juhudi za dharura za WFP nchini Afghanistan.
Ili kuendelea kutoa msaada, WFP inafanya kazi ya kuanzisha njia mbadala ya usafirishaji inayojulikana kama Lapis Lazuli Corridor inayounganisha Turkey, Georgia, Azerbaijan, Bahari ya Caspian na Turkmenistan kabla ya kufika Afghanistan. Hata hivyo, njia hii inachukua muda mrefu zaidi na ina gharama kubwa.
Watu wanaoingia Syria kutoka Lebanon waongezeka
Kwa upende wake Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, (UNHCR), linaripoti ongezeko kubwa la watu wanaoingia nchini Syria kutoka Lebanon kufuatia kuongezeka kwa mapigano.
Limesema Kati ya tarehe 2 na 13 Machi, takribani watu 118,500 waliingia Syria, wengi wao wakiwa ni raia wa Syria waliorejea nyumbani, ingawa baadhi ya raia wa Lebanon pia walivuka mpaka.
UNHCR kwa kushirikiana na WFP na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wameongeza misaada ya dharura katika vituo vya mpakani.
Mamlaka pia zimepeleka wafanyakazi zaidi katika maeneo ya kuvuka mpaka, hasa katika eneo la Joussieh, kufuatia ongezeko la mashambulizi ya anga nchini Lebanon.
Wapalestina wengi katika jumuiya tisa katika Ukingo wa Magharibi wamehamishwa kutokana na mashambulizi sasa mnamo 2026.
OHCHR yakemea mauaji ya familia za Wapalestina
Nayo Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, (OHCHR), katika eneo la Palestina linalokalibwa kwa mabavu na Israe imelaani mauaji ya familia mbili za Wapalestina yaliyofanywa na majeshi ya Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Huko Gaza, shambulizi la anga katika eneo la Az Zuwaida linaripotiwa kumuua mwanaume, mke wake mjamzito, mtoto wao mdogo na kijana mmoja aliyekuwa akijificha karibu. Kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, majeshi ya Israel yamewapiga risasi na kuwaua wanandoa pamoja na watoto wao wawili wadogo katika mji wa Tammoun.
Ofisi hiyo imesema matukio hayo yanaibua wasiwasi mkubwa kuhusu mwenendo unaoendelea wa mauaji yasiyo halali ya Wapalestina bila kuwajibishwa.
Ajith Sunghay mwakilisho wa Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu amesema “Kutokuwajibika kunasababisha mauaji zaidi, watu zaidi kufukuzwa makwao na mateso zaidi kwa Wapalestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Uwajibikaji kwa ukiukwaji wote wa haki za Wapalestina ni muhimu ili kubadili mwenendo huu wa kutisha.”
Wasichana wawili wa Palestina wanacheza katikati ya uharibifu katika mji wa Gaza
Muhtasari wa maendeleo muhimu yaliojiri wiki iliyopita
• Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa wito wa kusitishwa kwa vita wakati wa ziara yake ya mshikamano mwishoni mwa wiki mjini Beirut, akisisitiza kuwa “watu wa Lebanon hawakuchagua vita hivi,” na kuhimiza kusitishwa mara moja kwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah pamoja na kuongezwa kwa msaada wa kimataifa kwa serikali ya Lebanon.
• Mapigano kando ya msitari tenganishi baina ya Israel na Lebanon au Blue Line yameongezeka, yakihusisha mashambulizi ya makombora kuelekea Israel na mashambulizi makali ya anga ya Israel kusini mwa Lebanon na katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.
• Mgogoro wa watu waliolazimika kuyahama makazi yao umeongezeka zaidi katika kanda hiyo. Nchini Lebanon pekee, zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makazi yao kutokana na wiki kadhaa za mashambulizi ya anga na maagizo ya kuhama. Katika kanda nzima, mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, wakiwemo idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani nchini Iran.
• Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililoongozwa na Bahrain kuhusu mgogoro huo, huku rasimu nyingine ya azimio iliyoongozwa na Urusi ikishindwa kupata kura za kutosha.
• Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaongeza hatua za kibinadamu katika kanda hiyo. Umoja wa Mataifa umezindua ombi la dharura la dola milioni 308 kusaidia watu milioni moja nchini Lebanon, huku Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) likiongeza msaada kwa mifumo ya afya iliyoko katika shinikizo nchini Lebanon, Iraq na Syria.