
Nianze na wasilisho la Sara Hossain ambaye ni Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kimataifa ya Kusaka Ukweli kuhusu Iran, FFM iliyoundwa mwezi Novemba mwaka 2022 kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran.
Bi. Hossain ameonya kuwa raia wamenasa katikati ya mashambulizi ya kijeshi na ukandamizaji wa ndani ya nchi huku akirejelea uharibifu wa shule huko Minab uliotokana na shambulizi la siku ya kwanza lililofanywa na Marekani na Israeli na kuua zaidi ya watu 168 wengi wao wakiwa wanafunzi wa kike akiwemo mtoto wa umri wa miaka 7.
“Katika muktadha huu, tuna wasiwasi hasa kuhusu kauli za hadharani za maafisa wakuu wa Marekani zinazodokeza kwamba ‘kanuni za ushiriki katika mapigano’ zilizokuwepo kwa muda mrefu hazitumiki katika mzozo huu. Tunaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na pande zote katika mzozo huu, na kukusanya ushahidi.”
Mai Sato, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Iran yeye amemulika madhara ya vita hiyo kwa sasa na baadaye akisema, “zaidi ya raia 1,000 wameripotiwa kuuawa, shule ya msingi, hospitali na maeneo ya Urithi wa Dunia vimeshambuliwa na kuharibiwa. Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta yamesababisha athari mbayá za sumu kwa mazingira, na uwezekano wa madhara makubwa ya muda mrefu kwa afya ya umma; haya yote yakitokea katika nchi ambayo tayari ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.”
Kauli ya Iran imetolewa na Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi, Balozi Ali Bahreini ambaye akizungumza kwa lugha ya kiingereza badala ya kiajemi ilivyozoeleka, amegeukia jamii ya kimataifa.
“Leo hii ambapo zaidi ya maisha ya watu 1,300 wasio na hatia yamepotea, na zaidi ya watu 7,000 wamejeruhiwa, akiwemo mtoto wa mwenye umri wa miezi sita ambaye sasa anapigania maisha yake; jumuiya ya kimataifa haipaswi kubaki kimya.”