Homera aja na ‘Sema na Waziri’, asisitiza Katiba kipaumbeleHomera aja na ‘Sema na Waziri’, asisitiza Katiba kipaumbele

DODOMA: WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amezindua programu ya Sema na Waziri huku akisisitiza kuwa suala la Katiba Mpya bado ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, wamewataka wananchi kuwa na subira hadi hapo michakato miwili muhimu ya Tume ya Uchunguzi wa vurungu za Oktoba 29 na mchakati wa maridhiano itakapokamilika

Dk Homera ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati wa kuzindua programu ya ‘Sema na Waziri’ inayowezesha wananchi kuzungumza moja kwa moja na waziri kupitia njia ya simu ikiwa ni baada ya kuulizwa na mwananchi ambaye hakutaja jina lake kutoka Mkoa wa Geita aliyetaka kujua hatua zilizofikiwa katika mchakato wa uandishi wa Katiba Mpya.

Akijibu swali hilo, alisema kuwa katiba mpya bado ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Serikali awamu ya sita ya Awamu ya Sita na ni kipaumbele cha Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kuwa Serikali imejizatiti kulitekeleza.

“Uandishi wa katiba mpya ni suala muhimu kwa wananchi na ni sehemu ya ilani ya uchaguzi ya CCM. Hata hivyo, kwa sasa tunasubiri kukamilika kwa michakato miwili muhimu kabla ya kuanza rasmi uandishi wa katiba mpya.”
Dk Homera alisema kwa sasa unasubiriwa kukamilika kwa kazi ya Tume Huru ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo inatarajiwa kukamilisha majukumu yake na kuwasilisha ripoti huku mchakato wa pili ni maridhiano.

“Baada ya maridhiano, kinachofuata ni suala la katiba. Hivyo, nawasihi wananchi muwe na subira, kwani Rais hajaacha suala hili. Michakato hii miwili lazima ikamilike kwanza kabla ya mchakato wa katiba kuendelea.”
Kuhusu programu ya Sem ana Waziri, Dk Homera alisema huduma hiyo imelenga kuboresha utoaji wa huduma kwa watanzania na kuendelea kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa jamii ya Watanzania.

“Rais Samia alituelekeza kwamba lazima tuhakikishe kwamba wananchi wanasikilizwa na wanapata haki, kusikilizwa lazima tuwe na njia mbalimbali, tunayo Mama Samia Legal Aid, tunakituo cha huduma kwa wateja ambao inapokea malalamiko, changamoto ili wananchi waweze kusaidiwa.”

“Hii programu ya Sema na Waziri ni muendelezo kutekeleza maelekezo ya Rais kwamba lazima tuweze kusikiliza changamoto za wananchi na kutoa ufumbuzi hasa kwa masuala ya kisheria kwa namba.”
Dk Homera alisema kupitia programu hiyo atakuwa akizungumza na wananchi mmoja kwa moja mara tatu kila mwezi.

SOMA: Sera Msaada wa Kisheria mbioni kutungwa

“Kwa sasa ina maana wananchi wanaweza kuja kwa waziri, kukutana na wataalamu lwetu hapa wizarani lakini kubwa tumewapa fursa ya kupiga simu moja kwa moja na kupatiwa ufafanuzi,” alieleza

Akizungumza huduma ya kituo cha huduma kwa mteja kilichozinduliwa mwaka 2024, Dk Homera alisema malalamiko 2023 yamepokelewa kutoka kwa wananchi na kati ya hayo malalamiko 1,394 yameshughulikiwa na malalamiko 481 bado yanafanyiwa kazi na ufuatiliaji na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia mawakili wa serikali.

Alisema malalamiko yaliyopokelewa yanahusu ardhi, ndoa, talaka, kazi na ajira, mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na matunzo ya watoto.

“Hatutabakua changamoto zozote zile tutaendelea kuzipokea na kumwelekeza mwanchi aende wapi ili aweze kupata haki na yatakayotuhusu tutayashughulikia.”

Aidha, baadhi ya wananchi walipigasimu na kuzungumza na Waziri Dk Homera alipewa elimu na ushauri kuhusu mirathi na malezi ya mtoto katika kuziendea haki zao huku wengine wakishukuru namna huduma ya msaada wa kisheria ilivyowasaidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *