GENEVA: Tanzania imetoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha maendeleo ya kasi ya Akili Unde (AI) yanasimamiwa kupitia mifumo ya kimataifa iliyo jumuishi, yenye uwazi na usawa.

Pia imeonya kuwa nchi zinazoendelea hazipaswi kuachwa nyuma wakati teknolojia hiyo ikiendelea kubadili uchumi, utoaji wa huduma na maendeleo ya jamii duniani.

Akizungumza katika Mdahalo wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde (Global Dialogue on AI Governance) uliofanyika Geneva na kuhudhuriwa na zaidi ya wajumbe 190 kutoka serikalini, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na wadau wa teknolojia, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, alisema Tanzania imejipanga kutumia Akili Unde kama kichocheo cha maendeleo ya taifa huku ikihakikisha matumizi yake yanazingatia uwajibikaji.

Alisema Tanzania inaichukulia Akili Unde kuwa nguzo muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa kidijitali unaochipukia.

Kairuki alisisitiza kuwa maendeleo ya teknolojia hiyo yanapaswa kwenda sambamba na sera na mifumo madhubuti ya utawala itakayohakikisha manufaa yake yanawafikia watu wote kwa usawa, hususan katika nchi zinazoendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *