Kwa mujibu wa FAO eneo hilo la Mashariki ya Kati lina mchango mkubwa katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea duniani, hivyo mgogoro huu unaoendelea unaweza kuvuruga kabisa uzalishaji wa chakula kwa muda mfupi na na kwa muda mrefu. Maximo Torero ni mchumi mkuu wa FAO anasema
“Asilimia 30 hadi asilimia 35 ya mbolea ya dunia inatoka katika Ukanda huu, asilimia 30-35 ya amonia pia na asilimia 30 ya biashara ya mbolea inapiatia mlango baharí wa Hormuzi hivyo sio tu athari kwa leo lakini pia athari kwa kesho.”
Mchumi huyo mkuu wa FAO, Torero, amesisitiza kuwa kupanda kwa bei ya mbolea tayari kunazidi asilimia 20 hali inayoweza kupunguza uzalishaji wa mazao katika misimu ijayo ya kilimo.
Timu ya FAO ikifanya ziara ya shamba ya njugu mawe ambayo ni chanzo kikuu cha protini na chakula cha miongo mingi nchini Lebanon.
FAO inaonya kuwa iwapo mgogoro huu utaendelea, basi athari zake zitakuwa kubwa zaidi na za muda mrefu katika uzalishaji wa chakula duniani.
“Iwapo hali hii itaendelea kwa zaidi ya miezi mitatu athari zitakuwa mbayá sana, itaathiri kwa kiasi kikubwa msimu ujao wa upandaji, na hilo litakuwa na athari za muda mrefu.”
Hii ina maana kuwa sio tu bei za vyakula zitapanda, bali pia uzalishaji wa baadaye unaweza kupungua, na kuongeza hatari ya uhaba wa chakula duniani.
Torero ameeleza kuwa nchi kama Iran, ambayo tayari ilikuwa na changamoto za uhaba wa chakula, itaathirika zaidi.
“Hivyo matarajio ni kwamba bei za chakula Iran zitazidi kupanda na hii itaongeza shinikizo kubwa kwa ambayo tayari ni hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula.”
Kwa mujibu wa FAO kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama ngano, unga na mchele kunatarajiwa kuongeza shinikizo kwa familia zilizo hatarini.
hivyo inasisitiza umuhimu wa kutafuta njia mbadala za usafirishaji, kudhibiti masoko, na kusaidia wakulima kwa muda mfupi ili kupunguza athari.
Shirika hilo pia linaonya kuwa bila hatua za haraka za kuzuia kuongezeka kwa mgogoro, athari zake kwa uhakika wa chakula duniani zinaweza kuwa kubwa na za kudumu.