
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Luteni Jenerali Hatami amesema kuwa jibu la Iran kwa mauaji ya kigaidi ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa litakuwa thabiti na la kuwafanya wahusika wajute.
Jenerali Hatami ametoa ujumbe akilaani kitendo hicho cha kigaidi na cha kihalifu kilichofanywa na utawala wa Kizayuni pamoja na Marekani, na akatoa pongezi za shahada na rambirambi kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa taifa tukufu la Iran, na kwa familia ya shahidi mpendwa Dkt. Ali Larijani, aliyekuwa Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Ameongeza kuwa, wasifu wa huduma wa shahidi huyo mtukufu umejaa mchango muhimu katika nyanja mbalimbali za uongozi, utungaji sera na mikakati ya kitaifa. Nafasi muhimu alizoshika Dkt. Larijani katika majukumu makubwa ya kitaifa, hasa akiwa mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, zinaonesha wazi imani ambayo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uliweka katika uwezo na ustahiki wake wa kusimamia masuala nyeti na ya hatima ya taifa. Jenerali Hatami amesema bila shaka, busara, hekima na mtazamo wake uliojengwa juu ya mantiki ya mapinduzi umeacha athari nyingi za kudumu kwa taifa letu pendwa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba kitendo hiki cha kinyama, cha kigaidi na cha kukata tamaa katu hakitaweza kudhoofisha azma isiyotikisika ya taifa kubwa la Iran katika kulinda uhuru, kujitegemea, mamlaka ya ardhi na mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema, watu wa Iran, wakifuata njia ya kujitolea na shahada, na wakiongozwa na mafundisho na maelekezo ya Maimamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wataendelea kwa azma kubwa zaidi kusonga mbele katika njia ya malengo ya juu ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Amehitimisha kwa kusema kwamba, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwa kutumia uwezo wa kimkakati na wa ulinzi tulionao, katika wakati na mahali muafaka, jibu thabiti, la kuzuia na la kuwafanya wajute litatolewa dhidi Marekani ya mtenda jinai na utawala wa Kizayuni wenye kumwaga damu. Bila shaka kisasi kwa damu takatifu ya shahidi huyu mtukufu pamoja na mashahidi wengine wa thamani kitachukuliwa.