Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Thameen Al-Kheetan, amesema uwajibikaji ni muhimu na waathiriwa hawapaswi kusahaulika.

“Mlipuko wa kusikitisha wa jana usiku lazima uchunguzwe kwa haraka, kwa uhuru na kwa uwazi, na wale waliohusika wawajibishwe kwa mujibu wa viwango vya kimataifa,” amesema akiongeza kuwa “Waathiriwa na familia zao wana haki ya fidia.”

Uharibifu mkubwa eneo la tukio

Mashuhuda wa tukio hilo wameelezea hali mbaya baada ya mlipuko huo, wakisema kulikuwa na uharibifu mkubwa katika kituo hicho cha afya.

“Mashuhuda walielezea eneo la hospitali lilivyoharibiwa kabisa, na mamia ya watu wakitafuta ndugu zao,” ameongeza Al-Kheetan.

Ukubwa wa uharibifu huo umeibua hofu kuhusu usalama wa raia na mashambulizi dhidi ya maeneo yanayolindwa.

Ulinzi wa raia chini ya sheria za kimataifa

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, ikiwemo vituo vya afya, yamepigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.

“Raia na mali za kiraia zinapaswa kulindwa kikamilifu,” amesema msemaji huyo.
“Shambulio lolote lazima lizingatie kanuni za msingi za kutofautisha walengwa, uwiano na tahadhari na sheria za kimataifa zinatoa ulinzi maalum na wa ziada kwa vituo vya afya.”

Idadi ya waathiriwa yaongezeka huku mapigano yakizidi

Mlipuko huo umetokea wakati mvutano unaongezeka kati ya Pakistan na Afghanistan.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa karibu raia 300 wa Afghanistan wameuawa au kujeruhiwa katika wiki za hivi karibuni.

“Tangu mapigano yalipozidi kushika kasi mwishoni mwa mwezi uliopita, raia 289 wa Afghanistan, wakiwemo watoto 104 na wanawake 59, wameuawa au kujeruhiwa,” amesema Al-Kheetan.

Makumi ya maelfu ya watu pia wamekimbia makazi yao, hasa kusini na kusini-mashariki mwa Afghanistan.

Wito wa kusitishwa kwa mapigano na msaada wa kibinadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa wito kwa pande zote kupunguza mvutano na kulinda raia.

“Pande zote lazima zichukue hatua madhubuti kuhakikisha ulinzi wa raia na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wanaohitaji kwa dharura,” amesema msemaji huyo.

Nchini Pakistan, pia kuna ongezeko la watu waliolazimika kuyahama makazi yao, huku shule zikifungwa katika maeneo yaliyoathirika.

Umoja wa Mataifa sasa unatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, ukionya kuwa bila hatua za haraka, hali ya kibinadamu inaweza kuwa mbaya zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *