Video iliyorekodiwa na UNMISS, inamwonesha Afisa Wafaa, kama zilivyo asubuhi nyingine,
amesimama mbele ya mlango wa chumba chake katika eneo la malazi ya walinda amani. Siku huanza kwa mkutano wa timu nzima ya Polisi wa Umoja wa Mataifa (UNPOL), kupanga maeneo ya kuimarisha ulinzi kwa raia.
Wafaa Assri Sameeh Al-Goussous, Afisa Polisi wa UNMISS kutoka nchini Jordan, anafanya kazi ya kujenga uaminifu na uhusiano madhubuti kati ya jamii nchini Sudan Kusini.
Mara baada ya kumaliza mipango ya ofisini, sasa Afisa Wafaa anaelekea sokoni, baada ya kufika anatembea katikati ya vibanda na kuzungumza na akina mama na mabinti wanaouza mboga. Anatoa elimu ya afya na usafi, kisha anatoka nje ya soko na kueleza:
“Nilikuwa nikizungumzia afya na usafi, kwa sababu unazungumza na mwanamke ambaye ni mama wa nyumbani, mtu anayetunza watoto wake na familia yake. Kwa hivyo anahitaji kudumisha afya na usafi wa kila mtu.”
Safari yake inaendelea hadi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani, IDP, ambapo anajumuika na watoto karibu na bomba la maji, anachukua sabuni na kuanza kunawa mikono yake kwa vitendo huku watoto wakimtazama. Anatabasamu kwa furaha anapowaona nao wakijitokeza kunawa mikono yao, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea utamaduni wa usafi. Anaelezea umuhimu wa kitendo hicho akisema “Leo tumewafundisha jinsi ya kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji… ukiisafisha mikono yako kwa sabuni na maji, unaweza kuua asilimia tisini na saba ya vimelea.”
Wakimbizi wa ndani na wakazi wa Bentiu Sudan Kusini wakichota maji kutoka kwa mfereji.
Jukumu la Wafaa haliishii kwenye afya pekee; anahitimisha siku yake kwa kukutana na Vikundi vya ulinzi wa jamii. Akiwa amesimama na kundi la wanaume na wanawake wa eneo hilo, anachukua ripoti na kubadilishana taarifa kuhusu hali ya ulinzi mitaani ili kusaidia kupanga doria za usalama.
Baada ya siku ndefu, Afisa Wafaa anahitimisha majukumu yake kwa tabasamu, akisema, “hivi ndivyo tunavyomaliza siku yetu. Natazamia kurejea kwenye malazi yangu, nile chakula, nioge, kisha nipumzike kidogo. Ahsanteni, na kwaherini!”
Hali hii inatoa picha ya upande wa kibinadamu wa walinda amani wa UNMISS hapa Bentiu, ambao licha ya mazingira magumu ya kazi, wanadhihirisha kuwa ulinzi wa amani unajengwa kupitia elimu, ukaribu na jamii, na ushirikiano.