Hakika hali inazidi kuwa tete Mashariki ya Kati. Mathalani nchini Lebanon, hali inasemwa imefikia kiwango cha kutisha. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya anga yanayoendelea na amri za kuondoka katika maeneo mbalimbali nchini humo. Mamia ya watu wanaripotiwa kupoteza maisha. Mratibu Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Imran Riza, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X ameonya kuhusu kuzorota kwa hali hiyo akisema: “Kiwango cha mateso ya kibinadamu nchini Lebanon kinaongezeka kadri mapigano yanavyoendelea. Familia zimekimbia makazi yao, huduma zimevurugika, na watoto wanaathirika zaidi.” Kisha akaambatanisha picha ya dawati la mwanafunzi likiwa tupu na nguo za watoto zikiwa zimeanikwa tu.

Wakimbizi

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR ofisi ya Lebabon limeeleza kwa masikitiko kuwa maeneo ya Beirut ambayo watu wengi walikimbilia kwa ajili ya usalama sasa yanashambuliwa. Raia hawapaswi kulengwa, wanapaswa kulindwa wakati wote, UNHCR imesisitiza.

media:entermedia_image:b9170dd9-0191-4ff3-92fe-57e219921587

© WFP/Jaber Badwan

Mwanamke hubeba mgao wa chakula unaosambazwa na Mpango wa Chakula Duniani huko Almaghazi, Gaza.

Chakula

Licha ya changamoto hizi, mashirika kama Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP yanajitahidi kuongeza juhudi za kutoa msaada wa dharura, ikiwa ni pamoja na chakula na huduma muhimu kwa waathirika…huyo ni Anne Vallande Naibu Mkurugenzi wa WFP Leabanon akieleza kuwa wako katika Kijiji cha Rmeich kilichoko mpaka wa kusini wa Lebanon wameleta vyakula, magodoro, maji na mahitaji mengine  ya wanawake na watoto.

Nyuklia

Wakati huo huo, wasiwasi kuhusu usalama wa nyuklia unaongezeka nchini Iran ambako leo ni siku ya 19 tangu nchi hiyo ilipoanza kushambuliwa na Marekani na Israel. Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA limeeleza kwamba jana jioni kombora lilipiga eneo la kituo cha nyuklia cha Bushehr. Ingawa hakuna uharibifu wala majeruhi walioripotiwa, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, ametoa wito wa “kujitahidi kwa kiwango cha juu kujizuia” ili kuepusha hatari ya ajali ya nyuklia.

Usafiri na mabaharia

Mgogoro huo pia unaathiri usalama wa usafiri wa baharini duniani. Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafirishaji Majini, IMO linaripoti kuwa mashambulizi dhidi ya meli karibu na Mlango wa Hormuz yamesababisha vifo vya mabaharia wasiopungua saba, huku wengine wakijeruhiwa. Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez, katika kikao kisicho cha kawaida cha Baraza la shirika hilo kinachofanyika leo na kesho jijini London, Uingereza amewaambia wajumbe wasiwasi wake mkubwa na huzuni kuhusu mashambulizi haya…akisema, “ Takriban mabaharia 20,000 bado wamekwama baharini wakikabiliwa na hatari kubwa na msongo wa mawazo.” Akaongeza kuwa hali hii inaathiri “uchumi wa dunia na uhakika wa chakula,” na hivyo akasisitiza umuhimu wa uhuru wa usafiri wa baharini.

Tags: Mashariki ya Kati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *