Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na António Costa Rais wa Baraza la Muungano wa Ulaya mjini Brussels, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataigfa ametoa ujumbe muhimu na wa dharura kwa wahusika wakuu wa mgogoro huo.
Ni Wakati muafaka kumaliza vita hivi
Akianza na Marekani na Israel, Katibu Mkuu ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, akionya juu ya madhara makubwa ya mzozo huo akisema
“Ni wakati muafaka kumaliza vita hivi ambavyo viko hatarini kutodhibitiwa kabisa, vikisababisha mateso makubwa kwa raia.”
Amesisitiza kuwa athari za mgogoro huo si za kikanda tu bali za kimataifa
“Athari zake katika uchumi wa dunia ni za kutisha, zikiwa na uwezekano wa kusababisha madhara makubwa hasa kwa nchi zenye maendeleo duni.”
Onyo kali kwa Iran
Katibu Mkuu pia ametoa ujumbe mkali kwa Iran, akiitaka kusitisha mashambulizi dhidi ya nchi jirani.
“Acheni kushambulia majirani zenu, hawakuwa sehemu ya mgogoro huu.”
Ameongeza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tayari limechukua msimamo “Baraza la Usalama limelaani mashambulizi haya na kuamuru yasitishwe.”
Kufungwa kwa mlangobahari wa Hormuz kunaathiri biashara kwa kiwango cha kimataifa.
Mgogoro wa Mlango Bahari wa Hormuz waongeza shinikizo duniani
Moja ya wasiwasi mkubwa uliotajwa ni kuendelea kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa kimataifa.
Guterres amesema “Kufungwa kwa muda mrefu kwa Mlango bahari wa Hormuz kunasababisha mateso makubwa kwa watu wengi duniani ambao hawahusiki na mgogoro huu.”
Hali hii amesema imeongeza hofu kuhusu usambazaji wa nishati, biashara na kupanda kwa gharama duniani.
Diplomasia ichukue nafasi ya vita
Katika wito mpana zaidi, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa sheria za kimataifa na diplomasia.
“Ni wakati wa nguvu ya sheria kushinda sheria ya nguvu. Ni wakati wa diplomasia kushinda vita.”
Ushirikiano wa EU na UN wasisitizwa
Katibu Mkuu pia amesifu ushirikiano kati ya Muungano wa Ulaya EU na Umoja wa Mataifa, akiuuita wa “kipekee.”
Ameeleza kuwa ana imani EU itachukua nafasi muhimu katika kujenga utaratibu na utulivu wa kimataifa unaozingatia sheria, haki, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na usimamizi wa teknolojia mpya.
Kauli hizi zinakuja wakati wasiwasi wa kimataifa unaongezeka kuwa kuendelea kwa mgogoro huo wa Mashariki ya Kati kunaweza kusababisha hali mbaya zaidi, yenye athari kubwa za kibinadamu na kiuchumi duniani.