Hata hivyo, makubaliano mapya yaliyofikiwa na makundi ya kisiasa yameleta “wakati wa matumaini na maendeleo” kwa watu wa Haiti.

media:entermedia_image:cbcd6853-21f7-404d-a0c2-60ecbfd3f4fb

© UNOCHA/Giles Clarke

Gari lililoteketea limesalia taka kando ya barabara katika mtaa katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.

Safari ya kurejesha Demokrasia na usalama

Katika ripoti iliyotolewa Machi 16, 2026 mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Carlos Ruiz Massieu, amesema kuwa Mkataba mpya wa Kitaifa wa Utulivu na Uratibu wa Uchaguzi ni hatua kubwa ya kisiasa.

Mkataba huu umelenga vipaumbele vya raia wa Haiti ambavyo ni kurejesha usalama, kuandaa uchaguzi wa kuaminika, na kusimamisha tena utawala wa kidemokrasia. Serikali thabiti imetajwa kuwa hitaji la lazima ili kuboresha maisha ya watu ambao wameathiriwa vibaya na mauaji ya zaidi ya watu 8,100 yaliyorekodiwa mwaka 2025 pekee.

Vyama 300 vya siasa kushiriki uchaguzi

Imeripotiwa kuwa takriban vyama na makundi ya kisiasa 300 yamejisajili kushiriki katika uchaguzi huo, jambo linaloonesha kiu ya mabadiliko. Mara ya mwisho nchi hiyo kufanya uchaguzi ilikuwa kati ya mwaka 2015 na 2017, na tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mwaka 2021, nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na tawala za mpito.

media:entermedia_image:9edcf972-83d9-4e92-97c9-2d8818899346

MINUSTAH/Logan Abassi

Alama ya wino kwenye kidole gumba inaonesha kwamba mpiga kura huyu nchini Haiti alienda kupiga kura mwaka wa 2016. (Maktaba).

Kwa nini hali bora ya kisiasa ni muhimu?

Ghasia za magenge ya wahalifu nchini humo zimesababisha takriban watu milioni 1.5 kukimbia makazi yao, huku hali ya kiuchumi ikizidi kudorora na kuongeza umaskini uliokithiri. Hivyo, suluhu yoyote ya kudumu ya kisiasa lazima iongozwe na raia wenyewe, huku mamlaka zikisaidiwa kuandaa uchaguzi wa madiwani, wabunge, na rais. Waziri Mkuu wa sasa wa Haiti, Alix Didier Fils-Aimé, ameripotiwa akisema kuwa uchaguzi huo utafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu ili kuhitimisha kipindi kirefu cha mpito.

Jumuiya ya kimataifa inasema nini?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likishirikiana na mashirika ya kikanda kama Jumuiya ya nchi za eneo la Karibea, CARICOM, limekuwa likihimiza wadau wote wa Haiti kufikia mwafaka wa muundo wa utawala wa baadaye. Juhudi za kimataifa zimeelekezwa pia katika kurekebisha mfumo wa mahakama ili kupambana na rushwa, ghasia za magenge, na uhalifu wa kijinsia ambao umekuwa silaha ya kuwanyanyasa wanawake na wasichana.

Msichana mchanga amesimama katika kambi iliyojaa watu, ya muda huko Haiti, akiwa amezungukwa na mahema na ndoo, akikazia hali ngumu za maisha zinazokabiliwa na familia zilizohamishwa.

© WFP/Maria Gallar

Familia zilizofurshwa na ghasia zinahifadhiwa katika mazingira yenye msongamano mkubwa na yasiyo safi katika shule moja huko Port-au-Prince.

Je, ni lipi jukumu la Umoja wa Mataifa?

  • Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu nchini Haiti, BINUH imepewa jukumu la kuratibu mazungumzo ya kitaifa na kusaidia mchakato wa katiba ili kuhakikisha kukabidhiana madaraka kwa amani.
  • Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama lile la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, (UNDP), la Kuhudumia Watoto (UNICEF), na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), yameendelea kutoa misaada ya kibinadamu na kimaendeleo nchini Haiti.
  •  Umoja wa Mataifa umesaidia katika ubunifu wa mpango wa kitaifa wa kupokonya silaha na kuwarejesha wapiganaji kwenye jamii (DDR), kuratibu juhudi za kupunguza ghasia za kijamii, pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, ili kuimarisha ulinzi na uwajibikaji nchini humo.
Sanduku la kupiga kura limewekwa katika darasa lililotumiwa kama kituo cha kupiga kura wakati wa uchaguzi uliopita nchini Haiti. (file)

MINUSTAH/Logan Abassi

Sanduku la kupiga kura limewekwa katika darasa lililotumiwa kama kituo cha kupiga kura wakati wa uchaguzi uliopita nchini Haiti. (Maktaba)

Mwaka 2026 umebeba matarajio makubwa ambapo kalenda ya uchaguzi imepangwa kuanza kwa duru ya kwanza ya wabunge na Rais tarehe 20 Agosti, na duru ya pili kufanyika tarehe 6 Desemba. Ili kufikia malengo haya, ni lazima tofauti za kisiasa ziwekwe kando ili kuimarisha usalama na kuepusha anguko kamili la uchumi, huku kurejea kwa demokrasia kukitajwa kama ufunguo pekee wa kurejesha taifa la Haiti.

Fahamu zaidi kuhusu jukumu la BINUH na lile la UNSOH pamoja na jinsi zinavyofanya kazi pamoja hapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *