
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, José Manuel Albares, amesisitiza kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wameanzisha “vita vya upande mmoja” dhidi ya Iran na huo ni“ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.”
Aidha, ameitaka Umoja wa Ulaya kukataa uchochezi wa kijeshi na ujizuie kujitosa vitani bila busara.”
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Objective, Albares alitoa kauli hiyo sambamba na onyo kuhusu hatari ya kuibuka kwa “machafuko” kufuatia kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi), huku akitoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuimarisha umoja wao.
Amesema kuwa nchi za Ulaya zinazoshikamana na misingi ya Umoja wa Mataifa zinapaswa kuchagua kati ya “utaratibu wa kimataifa au hali ya kutokuwepo kwa utaratibu.”
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uhispania alisisitiza kuwa vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ni vya “upande mmoja” na vinawakilisha “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.”
Kuhusu mzozo wa sasa wa Mashariki ya Kati amesema: “Tunapaswa kuchagua kati ya sheria au kinyume chake ambacho ni nguvu ya mabavu; tunapaswa kuchagua kati ya amani au vita.”
Aidha amesema kwamba “raia wa Ulaya wanapaswa kutambua nguvu na uwezo wa Umoja wa Ulaya,” ili uwezo huo uweze “kubadilishwa kuwa hatua ya kisiasa yenye athari katika ngazi ya kimataifa.”
Wakati vita vya kichokozi vya na Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran vikiendelea, baadhi ya washirika wa Marekani kama vile Ujerumani, Italia, Japan na Uhispania wamekataa kushiriki katika aina yoyote ya operesheni za kijeshi katika Ghuba ya Uajemi.
Hivi karibuni, Kaja Kallas, anayehusika na sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, alitangaza kuwa hakuna nchi iliyo tayari kuweka maisha ya raia wake hatarini kwa kushiriki katika operesheni za kijeshi dhidi ya Iran.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sánchez ametangaza kwamba hataruhusu Marekani kutumia vituo vya kijeshi vya Rota (Cádiz) na Morón (Sevilla) kwa operesheni za mashambulizi dhidi ya Iran. Uamuzi huo umesababisha mvutano wa kidiplomasia kati ya Madrid na Washington, na hata kupelekea vitisho vya kiuchumi. Katika taarifa yake, Sánchez alifupisha msimamo wa serikali kwa maneno machache tu: “Hapana kwa vita.”
Mashambulizi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalianza asubuhi ya tarehe 28 Februari 2026 sawa na tarehe 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Uchokozi huo ulianza wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, kwa upatanishi wa Oman, yalikuwa yakiendelea.
Kufuatia kuanza kwa mashambulizi hayo ya kijeshi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kutekeleza hujuma za kulipiza kisasi.
Majeshi ya Iran yamelenga ngome za kijeshi na kijasusi za utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na kambi na vituo vya majeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi. Iran imetekeleza mashambulizi yaliyofanikiwa kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.