“Gharama ya kibinadamu ya vita hivi visivyo na tahadhari inatia wasiwasi mkubwa. Mapigano yanaendelea bila kujali athari za haraka na za muda mrefu kwa raia katika eneo zima,” amesema.

Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu mikubwa ya nishati sasa yamefikia hatua hatari, huku kukiwa na vitisho vya kuongezeka zaidi kwa mapigano.

“Ili kulinusuru eneo hili dhidi ya hatari kubwa na kuzuia vifo zaidi vya raia pamoja na uharibifu wa miundombinu muhimu ya umma, juhudi mpya za kidiplomasia ni muhimu sana.”

Madhara ya vita huko Ghuba yasambaa hadi Nepal

Mgogoro wa Mashariki ya Kati unaendelea kuleta athari mbaya hata nje ya eneo hilo, ikiwemo katika nchi kama Nepal ambayo inategemea sana kupeleka wafanyakazi wahamiaji katika nchi za Ghuba.

Katika mahojiano, Numan Özcan ameeleza jinsi hali ya kutokuwa na usalama, usumbufu wa safari, na shinikizo la kiuchumi vinavyoathiri vibaya wafanyakazi wahamiaji na familia zao.

Msaada waongezwa nchini Lebanon

Wakati mgogoro ukiendelea kuongezeka nchini Lebanon, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kuongeza utoaji wa misaada kwa kushirikiana na wadau wa kibinadamu na serikali.

Kwa mfano, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP, limetoa zaidi ya milo milioni 1.1 ya moto tangu mwanzo wa mwezi. Pia zaidi ya mgao 165,000 ya lishe ya dharura na virutubisho vimesambazwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, (UNHCR) nalo linaendelea kusambaza magodoro, mikeka ya kulalia, na mablanketi.

Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya vituo vya afya yanaongeza shinikizo katika mfumo wa afya. Tangu tarehe 2 Machi, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, limeripoti mashambulizi 33 yaliyosababisha vifo vya watu 31 na kujeruhi wengine 48.

WFP hutoa misaada ya chakula kwa familia za wakimbizi wanaoishi katika shule ya umma katika mji wa Tariq Jdide, Beirut, Lebanon. Wajitolea hutoa vikapu vya chakula kwa watu wazima na watoto.

© WFP/Khadija Dia

Mgao wa chakula kwa familia za wakimbizi wanaoishi katika shule katika mji wa Tariq Jdide, Beirut, Lebanon.

Mapigano makali Kusini mwa Lebanon

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon, UNIFIL, umeripoti kuendelea kwa mapigano makali ya ardhini na angani, pamoja na kuongezeka kwa uwepo wa majeshi ya Israel ndani ya eneo la Lebanon.

Kwa mujibu wa Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, mamia ya magari ya kijeshi ya Israel yameonekana karibu na Blue Line, ambalo ni eneo lisilopaswa kufanyika shughuli za kijeshi, na magari hayo ya kijeshi ni pamoja na vifaru na magari ya kivita.

Mnara wa uangalizi wa UN pia ulishambuliwa kwa risasi, na mabaki yake kumjeruhi askari wa kulinda amani.“Tunakumbusha wahusika wote wajibu wao wa kuhakikisha usalama wa walinda amani,” amesema Bwana Ha2, akisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano na kurejea kwenye mazungumzo.

UNFPA yaonya hatari kwa wanawake na watoto wachanga

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi (UNFPA), limesema vita vinavyozidi kuongezeka vinaharibu maisha ya wanawake na watoto, huku wajawazito na akina mama wapya wakiwa hatarini zaidi.

Usumbufu wa njia za baharini na kufungwa kwa anga umechelewesha usafirishaji wa vifaa muhimu vya kuokoa maisha, ikiwemo  hospitali za muda za uzazi na vifaa vya kujifungulia salama pamoja na msaada kwa manusura wa ukatili wa kingono.

Licha ya gharama kuongezeka na uhaba wa fedha, UNFPA inaongeza juhudi zake kwa kupeleka kliniki tembezi, kusambaza vifaa vya kiutu, na kudumisha maeneo salama.

“Hata katikati ya mgogoro, kila mwanamke lazima aweze kujifungua kwa usalama na kila mwanamke na msichana alindwe dhidi ya ukatili,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Diene Keita.

media:entermedia_image:c568ca83-07e2-4860-8458-de92e2d7ed84

UN Photo/John Isaac

Mlinda amani wa UNIFIL akizungumza na mkazi kwenye vilima vya kusini mwa Lebanon.

Mgogoro waweza kugharimu Kanda ya Kiarabu dola bilioni 150

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Jamii kwa Asia Magharibi, ESCWA, imeonya kuwa mgogoro huo unaweza kupunguza uzalishaji wa kiuchumi wa eneo hilo kwa hadi dola bilioni 150 ndani ya mwezi mmoja—sawa na asilimia 3.7 ya Pato la Taifa (GDP).

Makadirio ya awali yanaonesha hasara ya dola bilioni 63 ndani ya wiki mbili tu, kutokana na kuvurugika kwa masoko ya nishati, njia za biashara, usafiri wa anga, na mifumo ya kifedha.

Usafirishaji kupitia  Mlango wa baharí wa Hormuz umeshuka kwa asilimia 97, huku karibu safari za ndege 19,000 zikifutwa, hali inayoongeza shinikizo la kiuchumi.

“Madhara ya kiuchumi ya mgogoro yanaonekana haraka kupitia njia nyingi kwa wakati mmoja,” amesema Mkuu wa ESCWA, Mourad Wahba, akionya kuwa uchumi dhaifu unaweza kushindwa kustahimili mshtuko wa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *