
Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumza kwa simu na mwenzake wa Uingereza, Yvette Cooper, kuhusu taathira za vita vya kulazimishwa vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na hali ya mambo ya sasa katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Katika mazungumzo hayo, Araqchi ameeleza hatua za kiulinzi za Iran mkabala wa mashambulizi ya Marekani na Israel na kukosoa msimamo hasi na wa upendeleo wa Uingereza na baadhi ya nchi za Ulaya kuhusu mashambulizi hayo ambayo yamekiuka sheria za kimataifa.
Araqchi amesisitiza kuwa Iran ina haki kamili ya kujihami kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa: “Tumeheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi jirani na hatukuwa na lengo la kuwashambulia majirani zetu lakini kwa bahati mbaya kambi za kijeshi za Marekani zipo katika nchi hizo; na tunashambuliwa kutokea huko” amesema Sayyd Araqchi na kuongeza: Nchi hizo hazijatekeleza jukumu lao la kimataifa la kuzuia kutumiwa ardhi zao kuishambulia Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa vikali hatua ya Uingereza ya kuipatia Marekani kambi zake za kijeshi. Ameongeza kuwa bila shaka yoyote kitendo hicho ni kushiriki katika mashambulizi dhidi ya Iran na kitasajiliwa katika historia ya uhusiano wa nchi mbili.