
Mauaji ya kigaidi dhidi ya Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran mnamo Machi 17, 2026, siku 18 tu baada ya mauaji mengine ya kigaidi dhidi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Seyyed Ali Khamenei, ni zaidi ya suala la kuongezeka tu mashambulizi ya kijeshi. Yanaangazia wazi upuuzaji wa sheria za kimataifa zilizobuniwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia 1945.
Marekani na Israel zimechukua hatua ambazo zinakiuka wazi sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhusika kwao moja kwa moja katika jinai za kivita. Jambo la kusikitisha ni kwamba taasisi ambazo zimepewa jukumu la kutekeleza na kusimamia sheria hizi zikiongozwa na Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, zimenyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote ya kulinda sheria hizo, bali hata zimekuwa zikiunga mkono kimya kimya ukiukaji wake. Ukiukaji na upuuzaji huu wa sheria za kimataifa bila shaka unaakisi mantiki ya kiutendaji ya mfumo wa kimataifa, ambapo kujitawala kwa nchi kunategemea kufungamana na kutii kwake amri za madola yenye nguvu duniani.
Tarehe 28 Februari 2026, Marekani na Israel, zilianzisha vita na mashambulizi makali dhidi ya Iran, yakilenga viongozi wakuu wa nchi, miji mikubwa, miundombinu ya kiraia, na kusababisha vifo vya mamia ya watu na majeruhi. Shule ya msingi ya wasichana huko Minab ililengwa kwa makusudi ambapo wanafunzi 168 waliuawa kikatili, hospitali zilishambuliwa, na taasisi za Hilali Nyekundu ya Iran kuharibiwa. Mashambulizi haya yalimlenga kwa makusudi Kiongozi Mkuu, Ayatollah Seyyed Ali Khamenei- mwanasiasa wa kiraia na mkuu wa nchi, ambaye si mpiganaji katika uwanja wa vita.
Kifungu cha 2(4) cha Hati ya Umoja wa Mataifa kinapiga marufuku wazi wazi tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka ya nchi au uhuru wake wa kisiasa. Matumizi ya nguvu yanaruhusiwa tu katika hali ya kujilinda dhidi ya shambulio la silaha au kwa idhini ya Baraza la Usalama. Iran ilishambuliwa katika hali ambayo ilikuwa inashiriki kikamilifu katika michakato ya kidiplomasia, na wala haikuwa tishio kwa nchi yoyote, kama ilivyothibitishwa na Joseph Kent, mkuu wa zamani wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani, ambaye alijiuzulu kwa kupinga siasa za kichokozi na za kupenda vita za Rais Donald Trump, akisema Iran “haikuwa tishio kwa taifa letu.”
Ugaidi na ukiukaji huo wa sheria unaofanywa na Marekani na Israel dhidi ya viongozi wa Iran umeendelea kwa kuuawa Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa mnamo Machi 17. Larijani alikuwa shakhsia wa kisiasa na kiusalama, ambaye alikuwa na nafasi muhimu katika usimamizi wa majibu ya vita ya Iran. Mauaji yake ya kigaidi katika ardhi ya Iran bila shaka yanathibitisha kitendo cha uchokozi na jinai ya kivita.
Pamoja na hayo lakini kimya kimetanda katika ngazi za kimataifa. Tume Huru ya Kimataifa ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa kuhusu Iran, katika taarifa yake Machi 4, ililaani mauaji yasiyozingatia sheria na kusisitiza kwamba mauaji yanayolenga watu maalumu ni kinyume cha sheria. Baraza la Usalama halijachukua hatua yoyote kuhusu suala hili. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai nayo imekwepa kuchunguza wahusika wa mauaji hayo ya kigaidi. Ujumbe kwa Tehran na mataifa mengine huru uko wazi: Mamlaka ya kujitawala yanaheshimiwa tu pale yanapovumiliwa na kuruhusiwa na nchi za Magharibi.
Siasa hizi za kibaguzi zimekuwepo kwa miaka mingi. Suala hili linaonyesha wazi utaratibu wa kisheria ulioundwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya wenye nguvu duniani. Hati ya Umoja wa Mataifa inalinda rasmi mamlaka za nchi, lakini pamoja na hayo utekelezaji wa suala hilo unategemea kura ya turufu ya wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama. Wakati nchi inayotumia vibaya kura ya turufu inapokuwa yenyewe ndiyo chokozi, mfumo huo huwa umelemazwa kivitendo. Vitendo kama vile vya mauaji ya kigaidi dhidi ya Ayatollah Khamenei, Larijani na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Iran pamoja na kutekwa nyara Rais Nicholas Maduro ni thibitisho la wazi kuhusu madola makubwa kukiuka hadharani sheria za kimataifa bila kuwajibishwa na yeyote yule duniani.