Mwanazuoni mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatullah Sayyid Ali al‑Sistani, amelaani kwa maneno makali vita vinavyoendeshwa hivi sasa na Marekani na Israel dhidi ya Iran na Lebanon, na amewataka Waislamu wote pamoja na watu huru duniani kuvipinga na kuvikemea.

Katika ujumbe huo, mwanazuoni huyo aliwatakia waumini wanaume na wanawake Eid al‑Fitr yenye baraka, akibainisha kuwa sikukuu hiyo tukufu ni siku ya thawabu na siku ambayo Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, hujivunia waja Wake mbele ya malaika baada ya mwezi wa ibada na funga. Ametoa pongezi kwa waumini kwa kukubaliwa kwa ibada zao na kuomba sikukuu irudi kwa kheri na amani kwa Umma mzima.

Hata hivyo, amesema kuwa licha ya furaha ya Eid, nyoyo nyingi zimejaa huzuni kutokana na maafa, vita na mashambulizi yanayowakumba raia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Iran na Lebanon. Amesema kuwa wakati baadhi ya familia zinaadhimisha Sikukuu, kuna watoto wanaolia, mama wanaoomboleza, na nyumba zilizokuwa salama zikikumbwa na moto wa mapigano.

Mwanazuoni huyo amelaani vikali mashambulizi hayo na kutoa wito kwa Waislamu na jumuiya pana ya kimataifa kuonyesha mshikamano wao na kuunga juhudi za kusimamisha mapigano. Amewahimiza viongozi wa nchi na taasisi za kimataifa, hasa zile za Kiislamu, kutumia nafasi zao kuhamasisha mazungumzo na juhudi za kuleta utulivu.

Ayatullah Sistani amewaombea  waumini ulinzi, faraja na umoja, huku akiwaomboea mashahidi rehema na daraja za juu.

Mwanazuoni huyo ameisitiza kuwa imani ni zaidi ya kauli ni matendo, kusaidiana na huruma. Ametoa wito kwa waumini kuwasaidia walioathirika nchini Iran na Lebanon, kupitia njia zinazoaminika au kwa kusaidia wahitaji wanaojulikana moja kwa moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *