
Harakati ya Muqawama au mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon imeweka rekodi mpya baada ya kutekeleza operesheni 61 dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku moja.
Kwa mujibu wa Pars Today, wapiganaji wa Hizbullah nchini Lebanon wametekeleza operesheni 63 katika duru yao ya hivi karibuni ya mapambano dhidi ya adui Muisraeli katika vita vilivyopewa jina la “al‑Asf al‑Ma’koul”, ambapo operesheni 61 kati ya hizo zilitekelezwa siku ya Jumapili.
Hizbullah ilianza operesheni zake siku ya Jumapili saa kumi na mbili alfajiri kwa kulenga mkusanyiko wa wanajeshi wa adui katika kilima cha al‑Muhaysibat, kusini mwa mji wa al‑Taybeh.
Mlolongo wa operesheni za Hizbullah siku hiyo ya Jumapili ulijumuisha mashambulizi ya makombora ya kisasa, ndege zisizo na rubani, mizinga, roketi na mabomu, yakilenga vikosi vya adui, zana zao, miundombinu, makao makuu ya kijeshi pamoja na makazi ya walowezi wa Kizayuni. Aidha, kuliripotiwa pia mapambano ya moja kwa moja kati ya wapiganaji wa Hizbullah na vikosi vya adui katika baadhi ya makazi ya mpakani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, kina cha operesheni za Hizbullah ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kilifikia takribani kilomita saba siku hiyo ya Jumapili. Katika mashambulizi hayo, kituo cha ufuatiliaji na usimamizi wa operesheni za anga cha adui kilichopo kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kililengwa kwa makombora kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, operesheni ya mwisho ya Hizbullah siku hiyo ilifanyika saa kumi jioni, ambapo makazi ya Kizayuni ya Kiryat Shmona yalilengwa kwa wimbi la makombora na roketi.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa ni jukumu lake la kisheria na la kimaadili kulinda ardhi na wananchi wake, hususan wakati ambapo adui wa Kizayuni ameendelea kutenda ukatili na kuvuka mipaka na mistari myekundu mingi.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa Harakati ya Hizbullah inalenga tu ngome za kijeshi tofauti na adui wa Kizayuni ambaye hulenga raia wa kawaida.
Hizbullah imesema operesheni hizo ni wajibu wa chini kabisa unaopaswa kutekelezwa ili kuzuia adui kuendelea na jinai zaidi dhidi ya Lebanon, wananchi na harakati za Muqawama.