Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Tundaman (41), anafahamika na wengi kwa uwezo wake wa kuimba tangu akiwa na kundi la Tip Top Connection lakini kabla ya maarufu, safari yake ilikuwa ndefu na yenye changamoto nyingi.
Mkali huyo wa ngoma, Badman (2022) akishirikiana na Harmonize, alianza kuvutiwa na muziki akiwa bado mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Forodhani mnamo mwaka 2001.
Sasa akifahamika kutokana na umahiri wa nyimbo zake, Tundaman anasalia kuwa miongoni mwa wasanii walioweza kubadilika kulingana na ukuaji wa muziki, jambo linalomfanya kudumu katika tasnia.
Kipindi ndoto yake ya muziki imepamba moto, alikuwa akimkubali sana Ferooz kutokea kundi la Daz Nundaz, ambaye alimpa hamasa kubwa ya kuamini kuwa naye anaweza kufanya muziki na kufanikiwa.
Hata hivyo, msukumo mkubwa zaidi ulikuja siku ambayo Dully Sykes alifika shuleni kwao na kuimba wimbo wake ‘Julieta’ ambao ulitayarishwa na Miikka ‘Mwamba’ Kari kutokea Finland.
Tundaman alipousikia wimbo huo, alijikuta akiamini kwamba kipaji alichokuwa nacho kinaweza kumfikisha mbali zaidi, na hapo ndipo alipoanza kuuchukulia muziki kwa uzito zaidi.
Alianza rasmi kuipambania ndoto yake alipokutana na Matonya ambaye tayari alikuwa ameanza kujijengea jina kwenye muziki. Matonya alivutiwa na kipaji cha Tundaman na kumshauri waunde kundi ili iwe rahisi kwa wao kuvuma.
Kwa mujibu wa Tundaman, wazo hilo lilizaa wimbo wao wa kwanza ulioitwa Vailet (2006), ambao Tundaman alikuwa ameuandika tangu kitambo. Walienda kuurekodi katika studio za G Records chini ya Roy, mtayarishaji muziki aliyefariki mwaka 2008.
Ingawa Matonya alifanikiwa kurekodi sehemu yake kwa urahisi, Tundaman alipata changamoto kubwa kutokana na kutokuwa na uzoefu wa kurekodi. Mwishowe, aliamua kumuachia Matonya akamilishe wimbo huo peke yake, na ndipo ‘Vailet’ ulipokuja kuwa hit na kumtambulisha zaidi Matonya.
Ikumbukwe Matonya kwa mara ya kwanza alirekodi Motika Records, studio ya marehemu Mr. Ebbo, mara pili akarekodi kwa Miikka Mwamba aliyetengeneza wimbo uliomtoa kimuziki, Uaminifu (2003), hivyo alikuwa na uzoefu.
Baada ya mafanikio ya wimbo huo (Vailet), Matonya alianza kumchukua Tundaman na kwenda naye kwenye show mbalimbali, hata nje ya nchi kama Kenya.
Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwa Tundaman katika hatua hiyo, na ilibidi arejee Tanzania na kuanza upya kujipambania kivyake. Changamoto hizo hazikumvunja moyo, bali zilimjenga zaidi na kumuonyesha fursa.
Kwa haraka mambo yalibadilika alipofika Baucha Records na kukutana na Bob Manecky, mtayarishaji ambaye alimsaidia kurekodi wimbo wake, Neilah (2006). Manecky alimshauri amshirikishe msanii wa Hip Hop ili kuongeza uzito wa wimbo huo.
Mara moja Tundaman akapata wazo la kumshirikisha Professor Jay, ambaye walikuwa wakikutana mara kwa mara kwenye mechi za mtaani. Jay akaona nafasi hiyo ampe Chid Benzi ambaye alikuja kuitendea haki na matokeo yake yalikuwa mazuri kwani ‘Neilah’ ulikuwa wimbo mkubwa, na rasmi Tundaman akatambulisha kwa mashabiki.
Baada ya hapo, milango ya mafanikio ilianza kufunguka. Promota Bonga, ambaye pia alikuwa meneja wa Alikiba kwa wakati huo, alimpa Tundaman fedha nyingi kwa mara ya kwanza kutokana na show. Fedha hizo Sh400,000, ni kiasi ambacho hakuwahi kukishika kabla, hii ilionyesha wazi kuwa juhudi zake zilianza kuzaa matunda.
Hatua nyingine kubwa ilikuwa kujiunga kwake na kundi la Tip Top Connection, akishawishiwa na marehemu Abdu Bonge. Akiwa huko, aliulizwa ni wimbo gani alikuwa nao tayari, ndipo akautaja ‘Nipe Ripoti’ aliokuwa amepanga kumshirikisha Ferooz.
Hata hivyo, kutokana na changamoto za upatikanaji wa Ferooz kwa wakati linapokuja suala la show, iliamuliwa msanii mwingine achukue nafasi hiyo. Mwishowe, Madee alikuja kushirikishwa kwenye wimbo huo baada ya yeye kuupenda pia, na uliporekodiwa ukawa gumzo kubwa, ukabeba hata jina la albamu yake ya pili.
Kupitia albamu zake mbili ambazo ni Neilah (2007) na Nipe Ripoti (2009), Tundaman aliweza kujijengea heshima na hata kujitambulisha kama msanii mwenye uwezo wa kubadilika na kuendana na nyakati. Kutoka kwenye changamoto za kurekodi kwa mara ya kwanza hadi kuwa Tundaman huyu wa leo tunayemfahmu, anastahili pongezi.
Kwa miaka mingi Tundaman ameendelea kubadilisha aina ya muziki wake akiimba mahadhi mbalimbali kama Rege na Singeli, kitu kinachofanya kujizoelea mamilioni ya wasikilizaji wa nyimbo zake katika mitandao kama Boomplay Music na YouTube.
Hadi sasa ameweza kushirikiana na wasanii wenzake wengine wa Bongofleva kama Alikiba, Chege, Dulla Makabila, Abdukiba, Young Lunya, Kontawa, Toxic Fuvu, Balaa MC, Kayumba, Mabantu na kadhalika.