Kufuzu kwa timu za RS Berkane, FAR Rabat, Mamelodi Sundowns na Esperance katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kumefanya kurudiwa kwa historia moja ya kushangaza katika mashindano hayo.

Mechi za marudiano zilizochezwa za robo fainali ya mashindano hayo zilizochezwa, Jumamosi, Machi 21, 2026 na Jumapili, Machi 22, 2026 imezifanya timu hizo kuwa sehemu ya historia hiyo ngumu kujirudia katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

RS Berkane imepata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Al Hilal na kusonga mbele kwa ushindia wa jumla wa mabao 2-1, FAR Rabat imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pyramids FC na kutinga nusu fainali kwa mabao 3-2.

Al Ahly imechapwa mabao 3-2 na Esperance na kuondoshwa kwa mabao 4-2 huku Mamelodi Sundowns licha ya kuchapwa mabao 2-0 na Stade Malien, imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Kupenya kwa timu hizo kumefanya msimu huu kumefanya nusu fainali ya mashindano hayo msimu huu kushirikisha timu nne ambazo zote zilishika nafasi ya pili kwenye makundi yao huku zile zilizoongoza zikishindwa kufurukuta katika robo fainali.

Berkane ilikuwa ya pili katika kundi A lililoongozwa na Pyramids, FAR Rabat iliongozwa na Al Ahly katika kundi B, Mamelodi Sundowns kinara wake katika kundi C alikuwa ni Al Hilal na Esperance ilimaliza ya pili katika kundi D ambalo timu kinara ilikuwa ni Stade Malien.

Tangu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ilipoanza mwaka 2017 hadi sasa, ni mara mbili tu ambazo timu nne zilizoshika nafasi ya pili katika makundi, zote zilifanikiwa kuingia nusu fainali.

Ukiondoa msimu huu, mara ya kwanza kwa washindi wa pili wanne wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuingia kwa pamoja nusu fainali ilikuwa ni msimu wa 2019/2020.

Msimu wa 2019/2020, timu nne zilizomaliza katika nafasi ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilifanikiwa kutinga nusu fainali huku zilizoongoza zikikwamia katika robo fainali.

Timu hizo zilikuwa ni Zamalek na Al Ahly za Misri na Wydad Casablanca na Raja Casablanca za Morocco.

Zamalek ilishika nafasi ya pili katika kundi A lililoongozwa na TP Mazembe, Al Ahly ilimaliza ya pili katika kundi B ambalo kinara ilikuwa ni Etoile Du Sahel huku Wydad ikiwa ya pili kwenye kundi C ambalo bosi wake ilikuwa ni Mamelodi Sundowns na Raja iliongozwa na Esperance katika kundi D.

Kwenye robo fainali, Raja Casablanca iliitoa TP Mazembe, Zamalek ikaitupa nje Esperance, Wydad ikaifurusha Etoile Du Sahel na Al Ahly ikaiondoa Mamelodi Sundowns.

Katika msimu huo wa 2019/2020, timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni Al Ahly iliyoifunga Zamalek katika fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *