António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, wamezungumza leo (23 Machi) jijini New York, Marekani katika mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi amabayo huadhimishwa kila Machi 21.

Katibu Mkuu

Guterres amesema, “Ubaguzi wa rangi ni ukiukwaji wa haki za binadamu na utu wa binadamu. Ni tabia inayofundishwa ambayo imeenea sana na ina madhara makubwa.”

Pia amesema, anasikitishwa sana na jinsi ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni vinavyoanza kuonekana kama jambo la kawaida katika majukwaa ya kidijitali na mijadala ya kisiasa. Kinachoweza kuanza kama ishara fiche ujumbe wa siri unaolenga kuwahamasisha wabaguzi wengine kinaweza haraka kugeuka kuwa matamshi ya wazi ya chuki. Tunajua njia hii inaelekea wapi: katika dhuluma zaidi, vurugu, na hata mambo mabaya zaidi. Suluhisho ni mshikamano. Serikali, taasisi, biashara na jamii lazima zishirikiane kulinda utu, haki, usawa na haki za kila mtu.”

Rais wa Baraza

Rais wa Baraza Kuu yeye amesema, “mapambano dhidi ya ubaguzi wa aina zote, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi, hayamaliziki kamwe. Sio mahali tunapofika mara moja na kumaliza. Ni mchakato endelevu – uamuzi mmoja, hatua moja baada ya nyingine   unaohitaji uangalifu, uthabiti, na ujasiri.”

 

Kamishna haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu yeye amesema, “tumepiga hatua fulani katika safari ndefu kuelekea dunia yenye haki zaidi. Lakini tunakaribia hatua ya ukaguzi ambapo maendeleo haya yanahojiwa, kucheleweshwa, na hata kurudishwa nyuma. Hatua hii imewekwa na wale wanaonufaika na mgawanyiko na mgongano. Inaendelezwa na mifumo ya kibaguzi na kudumishwa na athari mbaya za kudhalilisha utu wa binadamu.”

Pia amesema, “rangi bado ndiyo msingi wa kawaida zaidi wa ubaguzi duniani. Hata hivyo, nchi nyingi bado hazina sheria za kupinga ubaguzi wa rangi, na hata robo ya nchi hazina sheria kamili za kupinga ubaguzi. Matamshi ya chuki yanaenea bila kudhibitiwa hata katika jamii zinazojivunia uvumilivu.”

Amesema, “katika ngazi ya kimataifa, mifumo yetu ya kisiasa na kiuchumi bado inaakisi karne nyingi za unyonyaji.”

Ameongeza, “tunahitaji kwenda zaidi ya maneno na kuchukua hatua kurekebisha mifumo ya zamani ya utawala wa kimataifa kiuchumi, kifedha na kisiasa ambayo imeibana dunia kwa kiasi kikubwa. Mataifa lazima yaweze kupata rasilimali wanazohitaji ili kutimiza haki za binadamu za watu wao, na pia yawe na sauti katika kuweka kanuni za uchumi wa dunia.”

Amehitimisha kwa kusema, “ubaguzi wa rangi sio tu ni kinyume cha haki na ni kinyume cha sheria; pia ni mufilisi kimaadili na kiakili. Kwa kuhoji mitazamo yetu, kuthibitisha ukweli, na kujifunza historia na haki za binadamu, tunaweza kuona kupitia mbinu za kupotosha na kutambua ubinadamu wetu wa pamoja. Kwa pamoja, lazima tuendelee kuvunja vizuizi vinavyowazuia watu hadi vitoweke kabisa. Kwa pamoja, tukabiliane, tukemee, na tuchukue hatua dhidi ya ubaguzi wa rangi kila wakati. Kuwa mpinga ubaguzi wa rangi haimaanishi kusimama na kundi moja dhidi ya jingine. Inamaanisha kusimama upande wa haki za binadamu na haki kwa wote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *