
Simiyu/Mara. Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na wadau wake, wakiwemo Benki ya Stanbic Tanzania na wadau wa Twende Butiama, wamekabidhi rasmi miundombinu ya vyoo katika shule mbili za msingi zilizopo mikoa ya Simiyu na Mara.
Shule zilizonufaika na mradi huo ni Shule ya Msingi Sima A iliyopo Bariadi mkoani Simiyu na Shule ya Msingi Madaraka iliyopo Butiama mkoani Mara, ambapo jumla ya matundu 20 ya vyoo vya kisasa yamejengwa, kumi kwa kila shule.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi iliyotolewa wakati wa msafara wa waendesha baiskeli wa Twende Butiama uliofanyika Julai mwaka jana, uliolenga kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na kuhamasisha maendeleo ya jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Vodacom Tanzania Plc, Ezekiel Nungwi, amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na jamii kuboresha mazingira ya elimu nchini.
“Kupitia Vodacom Tanzania Foundation tunaamini uwekezaji katika elimu ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa. Ujenzi wa vyoo hivi ni sehemu ya kutimiza ahadi yetu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira salama na bora ya kujifunzia,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sima A, Limi Subi, alisema mradi huo utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyoo na kuboresha afya za wanafunzi.
“Miundombinu hii ni msaada mkubwa kwetu. Itaboresha usafi wa mazingira ya shule na kusaidia wanafunzi kujifunza katika mazingira bora zaidi,” amesema.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Madaraka, Deocray Mtayomba, amesema ujenzi wa vyoo hivyo utapunguza muda unaopotea kwa wanafunzi kusubiri huduma hiyo, na hivyo kuongeza muda wa kujifunza.
“Tunawashukuru sana wadau kwa kutukumbuka. Hii itaboresha ustawi wa wanafunzi na kuongeza ufanisi wao darasani,” amesema.
Mbali na kuboresha miundombinu ya shule, mradi huo pia unalenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyoo bora na kuendeleza usafi wa mazingira.
Kupitia miradi yake ya kijamii, Vodacom Tanzania Foundation imeendelea kuwekeza katika sekta muhimu za maendeleo ya jamii, ikiwemo elimu, afya na mazingira, kwa lengo la kuchangia ustawi wa Watanzania na maendeleo endelevu.