
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amejibu madai ya uongo ya rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kuwepo kwa mazungumzo na Iran.
Mohammad Bagher Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Iran, ameandika kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X akijibu madai ya hivi karibuni ya Trump na kusema: “Watu wanataka wavamizi waadhibiwe kikamilifu kwa namna itakayowafanya wajutie.”
Alisisitiza pia kwamba: “Maafisa wote wa Iran wamesimama imara nyuma ya kiongozi wao na watu wao hadi lengo hili litakapofikiwa.”
Spika Qalibaf vilevile amesisitiza kuwa hakujakuwa na mazungumzo yoyote na Marekani, akisema: “Habari hizi za uongo zinalenga kupotosha masoko ya fedha na ya mafuta, na pia ni jaribio la kujitoa katika kinamasi ambamo Marekani na Israel wamekwama.”
Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha kuwepo mazungumzo yoyote baina ya Iran na Marekani katika siku 24 za hivi karibuni za vita vya kulazimishwa
Ismail Baqa’i, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amejibu swali kuhusu kusalimu amri rais wa Marekani baada ya vitisho dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran na kusema:
“Katika siku chache zilizopita, kupitia baadhi ya nchi rafiki, tumepokea ujumbe unaoonyesha ombi la Marekani la kuanzisha mazungumzo ili kumaliza vita. Majibu yanayofaa yametolewa kwa kuzingatia sera zetu za kimsingi.”
Ameongeza kuwa: “Katika majibu hayo, tumetoa maonyo muhimu kuhusu madhara makubwa ya jaribio lolote la kushambulia miundombinu muhimu ya Iran, na tumeweka wazi kwamba hatua yoyote dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran itakabiliwa na majibu ya wazi, ya haraka na yenye ufanisi kutoka kwa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Msemaji huyo mbali na kukanisha kikamilifu kuwepo kwa mazungumzo au mawasiliano yoyote na Marekani katika kipindi cha siku 24 tokea kuanza vita vya kulazimishwa, amesisitiza kwamba msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Lango Bahari Hormuz na masharti ya kumaliza vita haujabadilika kabisa.