Akizungumza kupitia Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric leo mjini New York Marekani, Katibu Mkuu amenukuu takwimu kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO zikionesha kuwa tangu Aprili 2023 kumekuwa na zaidi ya mashambulizi 200 yaliyothibitishwa dhidi ya vituo vya afya, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000, na kusisitiza kuwa “pande zote lazima zizingatie wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu,” zinazolinda wahudumu wa afya pamoja na miundombinu ya kiraia.
Mapigano lazima yakome
Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, kupunguzwa kwa mivutano, na kurejea kwa mazungumzo kwa kushirikiana na wapatanishi akiwemo Mjumbe wake Maalum Pekka Haavisto ili kufikia usitishaji wa kudumu wa mapigano na mchakato wa kisiasa jumuishi unaoongozwa na Wasudan wenyewe.
Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono hatua za dhati za kumaliza vita hivyo.
Idadi ya Vifo yaongezeka: WHO
Idadi ya vifo kufuatia shambulio hilo imeongezeka hadi watu 70, huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakionya juu ya ongezeko kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au droni yanayolenga raia kote nchini humo.
Hospitali ya Kufundishia ya Al Deain, mji mkuu wa Darfur Mashariki, ilishambuliwa Ijumaa mwishoni mwawiki katika tukio linalotajwa kuwa moja ya matukio mabaya zaidi katika mzozo unaoendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha wanamgambo cha Msaada wa Haraka Rapid Support Forces (RSF) ulioanza Aprili 2023.
Kwa mujibu wa WHO, miongoni mwa waliouawa ni wanawake saba na watoto 13, huku idadi hiyo ikiongezeka baada ya juhudi za uokoaji na utafutaji. Watu 146 wamejeruhiwa, wakiwemo wagonjwa na ndugu waliokuwa wakiwasindikiza.
Maelfu ya watu wamefurushwa na machafuko kutoka El Fasher hadi Tawila kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea.
Kituo cha afya chageuka eneo la maafa
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni daktari mmoja na wauguzi wawili, hali inayoonesha hatari kubwa wanazokumbana nazo wahudumu wa afya katika maeneo ya vita.
Dkt. Hala Khudari, Naibu Mwakilishi wa WHO nchini Sudan amesema “Shambulio dhidi ya hospitali si tu shambulio dhidi ya jengo, ni shambulio dhidi ya watu wanaotafuta matibabu, dhidi ya wahudumu wa afya wanaohatarisha maisha yao kuokoa wengine, na dhidi ya uwezekano wa kuishi wakati wa majanga.”
Ameongeza kuwa “Sudan inakaribia kuingia mwaka wake wa tatu wa vita vya silaha, lakini mashambulizi dhidi ya huduma za afya yanaendelea,” akisisitiza kuwa “vituo vya afya, magari ya wagonjwa, wahudumu na wagonjwa vimekuwa vikilengwa mara kwa mara.”
Tangu kuanza kwa mzozo huo, zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, kwa mujibu wa WHO.
Huduma muhimu kwa mamilioni ya watu zasitishwa
Uharibifu wa Hospitali ya mafunzo ya Al Deain umeifanya kufungwa kabisa, na kuwaacha zaidi ya watu milioni mbili bila huduma muhimu za matibabu.
Dkt. Khudari ameonya kuwa wagonjwa sasa watalazimika kusafiri zaidi ya kilomita 160 kufika hospitali nyingine ya rufaa safari ambayo inaweza kuwa hatari kwa wale wanaohitaji huduma za dharura au maalum.
Hospitali hiyo ilikuwa ikihudumia wakazi wa Al Deain pamoja na maeneo mengine tisa ya Darfur Mashariki, hivyo kupotea kwake ni pigo kubwa kwa mfumo wa afya ambao tayari ni dhaifu.
Hospitali ya Al Fasher huko Darfur imeangamia kwa kiasi kufuatia mashambulizi ya makombora mwezi Oktoba. (Kutoka Maktaba)
Matumizi ya droni yaongeza vifo vya raia
Office of the United Nations High Commissioner for Human Rights (OHCHR) imesema kuwa bado haijajulikana nani hasa anahusika na shambulio hilo, lakini pande zote mbili za mzozo zinatumia droni kwa kiwango kikubwa.
“Tunatoa wito kwa pande zote kusitisha mara moja matumizi ya aina hii ya silaha,” alisema msemaji wa OHCHR, Marta Hurtado.
Ameonya kuwa ongezeko la matumizi ya droni mwaka huu linaonesha “athari mbaya ya silaha za kisasa na nafuu katika maeneo yenye watu wengi.”
Zaidi ya raia 500 waliuawa katika mashambulizi ya droni kati ya Januari 1 na Machi 15 pekee, wengi wao katika eneo la Kordofan.
Hatari ya kusambaa kwa mgogoro
Vurugu sasa zinaanza kuvuka mipaka ya Sudan. Hurtado amebainisha kuwa mashambulizi ya droni yanaongezeka katika maeneo ya mipakani, jambo linalozua hofu ya kuenea kwa mgogoro huo katika ukanda mzima.
Ametaja mashambulizi ya hivi karibuni karibu na mpaka wa Sudan na Chad, ikiwemo katika mji wa At Tina na eneo la mpakani la Tine nchini Chad, kufuatia mashambulizi ya ardhini ya RSF.
“Mashambulizi ya droni yanayoenea yanaongeza hatari ya mgogoro kuongezeka zaidi na kuwa na athari za kikanda,” ameonya.
Hospitali nyingi zimeharibiwa na mashambulizi nchini Sudan
Hofu ya uhalifu wa kivita yaongezeka
Maafisa wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi mkubwa kwamba mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanaweza kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
“Mifumo inayoendelea ya mashambulizi dhidi ya raia na uharibifu wa miundombinu ya kiraia inaibua wasiwasi mkubwa kuhusu uzingatiaji wa sheria za kimataifa na inaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita,” amesema Hurtado.
Pia ametoa wito wa kusitishwa kwa usambazaji wa silaha unaochochea mzozo huo, akisisitiza umuhimu wa kulinda raia na kuwawajibisha wahusika.
Mgogoro usio na mwisho
Wakati vita nchini Sudan vinakaribia kuingia mwaka wake wa tatu, shambulio la Hospitali ya Al Deain linabaki kuwa ukumbusho mchungu wa athari kubwa za kibinadamu pamoja na hatari zinazoongezeka za matumizi ya teknolojia za kisasa za kivita katika maeneo yenye watu wengi.