
Ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Sokoni FC, umeifanya Naliendele Star kuibuka bingwa wa Nanauka CRDB Cup mkoani Mtwara, michuano iliyoanza Februari 15, 2026 ikishirikisha timu nane kutoka maeneo yenye mkikusanyiko mikubwa ya wananchi hasa vijana kama vile stendi, sokoni, feri na vijiwe vya bodaboda.
Kutokana na ushindi huo, Naliendele Stars ambayo imetoa mchezaji bora, golikipa bora na mfungaji bora pamoja na ‘man of the match’ katika fainali, imejinyakulia kitita cha Sh1 milioni huku kila mchezaji katika vipengele tajwa akiondoka na Sh100,000 kutoka kwa wadhamini wa Nanauka Cup ambao ni Benki ya CRDB.
Akizungumza baada ya fainali hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Mbunge wa Mtwara Mjini ambaye ni Waziri wa Ofisi, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alisema michezo huiunganisha jamii na kutoa fursa za kiuchumi.
“Tunahitimisha ligi hii ambayo ilikuwa maandlaizi ya ligi kubwa zaidi ya Nanauka CRDB Jimbo Cup itakayoanza Juni mwaka huu. Ligi hii kubwa zaidi itajumuisha timu kutoka katika kila kata ya Jimbo la Mtwara Mjini. Itakuwa ni nafasi nzuri ya vijana wa jimbo letu kukutana, kufahamiana na kujadili mambo yao,” alisema Nanauka.
Nanauka alisema Nanauka CRDB Jimbo Cup nayo itadhaminiwa na Benki ya CRDB ambayo ameishukuru kwa kuendelea kuwa jirani na vijana wa jimbo lake na nchini kote kwa ujumla.
“Nafahamu Benki ya CRDB mnadhamini wa Kombe la Shirikisho linalolojumuisha timu kutoka nchini kote na taasisi yenu ya CRDB Bank Foundation inadhamini Ndondo Cup. Ligi hizi zote zinawakutanisha vijana kama inavyojidhihirisha hapa katika fainali hizi za Nanauka CRDB Cup. Nawapongeza sana kwa kujitoa kwenu katika kuwawezesha vijana,” alisema.
Katika mchezo huo wa fainali, Sokoni FC ilianza kupata, kisha Naliendele Stars ikasawazisha na kuongeza ikaifanya kwenda mapumziko ikiongoza 2-1. Hata hivyo, Sokoni FC iliweka mipango vizuri na kusawazisha katika dakika ya 71 na kufanya hadi mwisho matokeo kuwa 2-2, ndipo mshindi akaamuliwa kwa penalti.
Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Huduma kwa Vijana wa Benki ya CRDB, Mshindo Magimba, alisema vijana ndio nguvu kazi kubwa nchini inayohitaji kuendelezwa na Benki ya CRDB inafanya kila iwezalo kushiriki kufanikisha hilo.
“Benki ya CRDB tunaiishi kaulimbiu yetu ya Ulipo Tupo. Leo hii tunashirikiana nanyi hapa Mtwara kupitia Nanauka CRDB Cup laini Benki yetu inawafikia vijana nchini kote ili kuwaunganisha na kuwakumbusha umuhimu wa huduma za fedha katika shughuli zao za kila siku. Michezo inatoa fursa ya kujenga uchumi wa kijana na Benki ya CRDB tupo kwa ajili ya kuifanikisha safari ya kiuchumi kwa kijana yeyote kuanzia hapa Mtwara na nchini kote kwa ujumla,” alisema Magimba.
Kwa kushika nafasi ya pili, Sokoni FC imekabidhiwa Sh500,000 na Likombe FC iliyoshika nafasi ya tatu imeondoka na Sh300,000. Timu yenye nidhamu katika ligi hiyo ni Kiangu FC ambayo imezawadiwa Sh100,000.