
Rais Masoud Pezeshhkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif ambapo pande hizo mbili zimejadili uhusiano wa nchi mbili, matukio ya sasa katika kanda ya Magharibi mwa Asia na athari za vita haramu vya Marekani na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran kwa usalama na kanda na dunia nzima.
Rais Pezeshkian ameeleza athari mbaya za uchokozi na mashambulizi hayo na pia jinai zinazoendelea kufanywa na Marekani na Israel na kusema: Matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu kwa nchi za kanda hii yako wazi kabisa. “Tunazitaka nchi za Kiislamu zisiruhusu Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kutumia ardhi na suhula zao kushambulia Iran, na kama haziwezi kuzuia vita na uchokozi huo, jambo hilo litapanua vita na ukosefu wa usalama katika kanda nzima,” amesema Rais Masoud Pezeshkian.
Akizungumzia athari mbaya za mashambulizi ya Marekani na utawala haramu wa Israel kwa usalama na amani ya kanda ya Magharibi mwa Asia, na vilevile kwa usalama wa usafirishaji wa baharini katika Lango Bahari la Hormuz, Rais Pezeshkian amesema: Ukosefu wa usalama wa kulazimishwa katika Lango Bahari la Hormuz ni matokeo ya moja kwa moja ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel. Amesema: Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya jitihada za kuchukua hatua za lazima za kudhamini usalama wa safari za majini na kuvuka salama meli za mizigo katika lango hilo, na itatoa ushirikiano unaohitajika kwa ajili ya kuvusha meli za meli zisizomilikiwa au zisizokuwa na uhusiano na wachokozi na wahusika wa vita vya sasa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ametoa wito wa kufanyika jitihada jumuishi za nchi za kanda ya Asia Magharibi hususan nchi za Kiislamu kwa ajili ya kupunguza mvutano na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
Sambamba na kutilia mkazo haki halali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kujilinda na kujitetea, Shehbaz Sharif amesema: Pakistan daima itaendelea kuwa pamoja na serikali na taifa la Iran.