
Vifaa hivi ni rahisi kutumia, vinatumia betri, na vina uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa moja, jambo linalompa nguvu na matumiani Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, kueleza kuwa, “Vifaa hivi vipya vinaweza kuleta mapinduzi ya kweli kwa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kusogeza vipimo vya haraka na sahihi karibu na watu, kuokoa maisha, kuzuia maambukizi, na kupunguza gharama.”
Ubunifu wa vipimo na urahisi wa huduma
Vifaa hivi vipya havina gharama kubwa ikilinganishwa na mashine za zamani, na vinaweza pia kutumika kupima magonjwa mengine ikiwemo Virusi Vya UKIMWI (VVU), homa ya nyani (Mpox), na virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi (HPV).
Hii inamaanisha kuwa mgonjwa anaweza kupata huduma za magonjwa mbalimbali katika kituo kimoja bila kuhitaji kusafiri umbali mrefu. Aidha, mbinu mpya ya kuchanganya sampuli za watu kadhaa na kuzipima kwa pamoja, imependekezwa ili kuokoa muda na gharama, hususan katika maeneo yenye rasilimali chache, ili kuhakikisha huduma zinawafikia wengi kwa haraka zaidi.
Kila siku watu 3,300 hufariki dunia kwa Kifua Kikuu
Pamoja na mafanikio ya kuokoa maisha ya watu takriban milioni 83 tangu mwaka 2000, Kifua Kikuu bado ni miongoni mwa magonjwa hatari zaidi duniani ambapo kila siku zaidi ya watu 3,300 hupoteza maisha.
Changamoto kubwa imekuwa ni gharama kubwa za vipimo na utegemezi wa maabara kubwa zilizoko mijini, jambo linalochelewesha matibabu. Dkt. Tereza Kasaeva, Mkurugenzi wa Idara ya VVU na Kifua Kikuu ya WHO, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye mapambano haya.
“Kuwekeza katika Kifua Kikuu ni chaguo la kimkakati la kisiasa na kiuchumi, likizalisha hadi dola 43 za kimarekani kama faida ya kiafya na kiuchumi kwa kila dola moja inayotumiwa,” amesema Dkt. Kasaeva.
Wito wa Siku ya Kifua Kikuu 2026
WHO inahimiza:
- Kuimarishwa kwa mifumo ya afya inayomjali mgonjwa zaidi na kuhusisha uongozi wa jamii katika kila hatua.
- Kuongeza fedha za utafiti ambazo kwa sasa ziko chini ya kiwango kinachohitajika cha dola bilioni 5 kwa mwaka, hali inayochelewesha upatikanaji wa dawa na chanjo mpya.