Guterres amesema “katika siku hii tunaitwa kukabiliana na urithi huu. Kwa kukataa simulizi potofu za tofauti za rangi na uongo mchafu wa ubora wa watu weupe. Kwa kuvunja mifumo ya ubaguzi wa rangi mtandaoni, katika vyombo vya habari, mashuleni, kazini, katika siasa, na hata ndani ya nafsi zetu. Na kwa kufanya kazi kwa ajili ya ukweli, haki na marekebisho ya madhara yaliyosababishwa.”

Akifafanua zaidi kuhusu utumwa amesema mamilioni ya watu walichukuliwa kutoka katika familia na jamii zao barani Afrika na kusafirishwa kwa nguvu kuvuka Bahari ya Atlantiki. Na kwa walioweza kuhimili safari hiyo ngumu walifanywa watumwa katika bara la Amerika.

“Mamilioni wengine walizaliwa katika utumwa, wakinyonywa kikatili kwa kazi zao, na kunyimwa utu na haki zao za msingi. Tunawaheshimu kwa ustahimilivu wao wa kimya kimya na kwa vitendo vyao vya ujasiri vya kupinga ukandamizaji waziwazi.”

Sanduku la Kurudi, Ukumbusho wa Kudumu wa Kuwaheshimu Wahasiriwa wa Utumwa na Biashara ya Utumwa katika Bahari ya Atlantiki, iliyoko kwenye Uwanja wa Wageni wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

UN Photo/Rick Bajornas

Sanduku la Kurudi, Ukumbusho wa Kudumu wa Kuwaheshimu Wahasiriwa wa Utumwa na Biashara ya Utumwa katika Bahari ya Atlantiki, iliyoko kwenye Uwanja wa Wageni wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mfumo huo wa utumwa wa kimataifa uliendelea kwa zaidi ya miaka 400 na athari zake bado zinaonekana duniani hata leo.

“Unaonekana katika mifumo na taasisi zilizoundwa na kunufaika na utumwa wa kumiliki binadamu kama mali. Unaonekana katika pengo la kijamii na kiuchumi lililotokana na dhuluma za zamani. Na unaonekana katika upendeleo na ubaguzi unaopenya katika utamaduni wetu na kuathiri maisha ya watu wengi.”

Kupitia taarifa hiyo Guterres ameakaribisha hatua za awali zilizochukuliwa na baadhi ya serikali kukabiliana na athari za utumwa.

“Lakini hatua za ujasiri zaidi kutoka kwa nchi wanachama wengi zaidi bado zinahitajika. Ikiwemo kuweka ahadi za kuheshimu umiliki wa nchi za Afrika wa rasilimali zao wenyewe. Na kuchukua hatua katika kuhakikisha kuna ushiriki na ushawishi sawa wa nchi hizo katika mifumo ya kifedha ya kimataifa na katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Ameihimiza dunia kushirikiana kwa pamoja, katika kuweka ahadi ya kujenga dunia ambamo kila mtu anaishi na kustawi kwa heshima na utu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *