Akizungumza na waandishi wa habari  hii leo nje ya ukumbi wa Baraza la Usalama la jijini New York, Guterres amesema mzozo huo umefikia kiwango ambacho hata viongozi wenye uzoefu mkubwa hawakutarajia.
“Ni wakati wa kusitisha kupanda ngazi ya kuongezeka kwa mzozo, na kuanza kupanda ngazi ya diplomasia, na kurejea katika heshima kamili ya sheria za kimataifa,” amesema.

Wito kwa Marekani, Israel na Iran

Guterres ametoa ujumbe mkali kwa Marekani na Israel, akiwataka kusitisha vita mara moja.

Amesisitiza kuwa “Ni wakati wa kumaliza vita, wakati huu ambapo mateso ya kibinadamu yanaongezeka, idadi ya vifo vya raia inaongezeka, na athari kwa uchumi wa dunia zinazidi kuwa mbaya”.

Wakati huo huo, ameiitaka Iran kusitisha mashambulizi dhidi ya majirani zake, akibainisha kuwa Baraza la Usalama tayari limeyalaani mashambulizi hayo na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa urambazaji katika njia muhimu za bahari kama mlango Bahari za  Hormuz.

Ameonya kuwa kufungwa kwa muda mrefu kwa mlango huo muhimu wa bahari “kunaathiri usafirishaji wa mafuta, gesi na mbolea katika kipindi nyeti cha msimu wa upandaji duniani.”

media:entermedia_image:db1c2c57-3474-46f1-9e26-c2df20d92565

UN Photo/Eskinder Debebe

Jean Arnault ameteuliwa na Katibu Mkuu kuwa mjumbe wwake Maalum kwa mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati

Juhudi za diplomasia na matumaini ya mazungumzo

Katibu Mkuu amesema amekuwa akiwasiliana na viongozi na wadau mbalimbali katika eneo hilo na duniani kote katika wiki za hivi karibuni, akisisitiza kuwa kuna mipango kadhaa ya mazungumzo inayoendelea ambayo mafanikio yake ni muhimu.

Uteuzi wa mjumbe huyo maalum unalenga kuimarisha juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Mataifa katika kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo huo unaozidi kusambaa.

Raia wanabeba mzigo mkubwa wa vita

Guterres ameeleza kuwa raia kote katika eneo hilo na kwingineko wanakumbwa na madhara makubwa na wanaishi katika hali ya hofu na ukosefu wa usalama.
Amesema ameshuhudia binafsi athari hizo wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Lebanon.

Amesisitiza pia haja ya kusitisha mapigano nchini humo, akisema Hezbollah lazima isitishe mashambulizi dhidi ya Israel, huku Israel nayo ikitakiwa kusitisha operesheni zake za kijeshi na mashambulizi ya anga ambayo yanaathiri zaidi raia.
Ameonya kuwa “Mtindo wa Gaza haupaswi kurudiwa nchini Lebanon”.

Katibu Mkuu wa Un Antonio Guterres akienda kuzungumza na waandishi wa habari

UN Photo/Mark Garten

Katibu Mkuu wa Un Antonio Guterres akienda kuzungumza na waandishi wa habari

Athari za kiuchumi na kibinadamu duniani

Katibu Mkuu ameonya kuwa mzozo huo umevuruga masoko ya kimataifa, kudhoofisha operesheni za kibinadamu na kuwaathiri zaidi watu maskini na walio hatarini ambao hawawezi kustahimili mishtuko mingine.

Amesema mfumo wa Umoja wa Mataifa unaendelea kufanya kazi kupunguza athari za vita, lakini akasisitiza kuwa njia bora zaidi ni kusitisha mapigano mara moja.

Wito wa mwisho, amani badala ya vita

Guterres amehitimisha kwa kusisitiza kuwa vita si suluhisho la mgogoro huo.
Ametoa wito wa kurejea katika amani, diplomasia na heshima kamili ya sheria za kimataifa kama njia pekee ya kuondokana na hali hiyo inayozidi kuwa mbaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *