Umoja wa Mataifa leo umekuwa na tukio la kumbukizi ya siku ya kimataifa ya kukumbuka waathiriwa wa biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlanitiki ambapo nchi 123 wanachama wa Umoja huo wamepitisha azimio lililoandaliwa na mataifa 58 kutambua usafirishaji wa watu wa kiafrika na utumwa kwa misingi ya rangi ya waafrika kuwa uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu.
Nchi hizo 123 ni pamoja na zile wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilhali nchi 3 zilizopinga azimio ni Marekani, Israeli na Argentina. Nchi 52 hazikuonesha msimamo wowote.
Mwakilishi wa Marekani akizungumza baada ya kupiga kura ya kupinga azimio hilo amesema, “tunalaani makosa yoyote yaliyofanyika kuhusiana na utumwa kuvuka bahari ya Atlantiki, jangwa la Sahara na kwingineko, lakini tumepinga azimio kwa sababu hatuoni msingi wa kulipatia kiwango cha juu hivyo cha hadhi tukio hilo. Na zaidi ya yote kama ni fidia, fidia hiyo atalipwa nani,?” amehoji.
Rais wa Ghana aliwasilisha rasimu ya azimio mbele ya Baraza Kuu
Rais John Mahama wa Ghana akihutubia Baraza Kuu wakati wa siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.
Rasimu ya azimio hilo iliwasilishwa na Rais wa Ghana John Mahama ambaye ni Balozi wa Muungano wa Afrika wa Kuendeleza Hali ya Haki na Fidia. Azimio hilo namba A/80/L.48 limepatiwa jina kutambua usafirishaji wa watu waliokuwa watumwa kutoka Afrika na utumwa kwa msingi wa rangi ya watu wa kiafrika kama mojawapo ya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu.
Azimio hilo lililoandaliwa na mataifa 58 yakiwemo mataifa ya Afrika Mashariki, lina vipengele 16 vya utekelezaji ikiwemo kutambua usafirishaji huo wa watumwa kutoka Afrika kuwa uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu, kurejeshwa kwa mali za kitamaduni kutoka Afrika na zaidi ya yote kulipwa fidia.
Kauli ya Rais wa Baraza Kuu
Tukio la kumbukizi lilianza kwa Annalena Baerbock Rais wa Baraza Kuu kuitisha kikao na kisha kuelekea kwenye mimbari kutoa hotuba yake akirejelea simulizi ya mtumwa Oladuk Ekwano kutoka Nigeria ya sasa akielezea machungu ya safari ndani ya meli iliyowabeba.
Rais wa Baraza Kuu la UN Annalena Baerbock akitoa hotuba katika tukio la siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.
Anasema Makumi ya mamilioni ya wengine kama Egvano walinyang’anywa kutoka kwa familia zao, nchi zao na tamaduni zao, wakafanywa watumwa na kupelekwa kufanya kazi katika nchi za kigeni—kwenye mashamba ya pamba hapa Marekani, na kwenye mashamba ya miwa na kahawa katika makoloni yaliyodhibitiwa na Ulaya. Katika maeneo ambayo leo yanajulikana kama Brazili, Barbados, Jamaica, na maeneo mengine mengi. Wote wakiwa mbali na nyumbani, mbali na familia, mbali na maisha yao.
Tunatambua nchi zinazoomba radhi lakini hatua zaidi zahitajika
Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerejelea mateso waliyopata mamilioni ya waafrika waliotekwa nyara na kusafirishwa katika hali dhalili na kugeuzwa watumwa barani Amerika. Amesema kumbukumbu pekee haitoshi.
Amebainisha kuwa mfumo huo haukuwa tu ukatili wa zamani bali pia ulikuwa msingi wa miundo ya uchumi wa dunia ambayo madhara yake yanaendelea hadi leo katika mfumo wa ubaguzi wa rangi wa kimfumo na ukosefu wa usawa.
Katibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba katika tukio la siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.
Hotuba hiyo imesisitiza kuwa kumbukumbu pekee haitoshi. Badala yake, nchi lazima zikabiliane na dhuluma za muda mrefu zinazoendelea kuwaathiri watu wenye asili ya Kiafrika. “Kiini cha juhudi hizo, alisema, ni kutafuta ukweli, haki, na marekebisho, ikiwa ni pamoja na mijadala yenye maana na hatua kuhusu fidia,” amesema Katibu Mkuu.
Guterres anasema, “Ndiyo maana Muongo wa Pili wa Kimataifa kwa Watu wenye Asili ya Kiafrika na Muongo wa Fidia wa Muungano wa Afrika ni muhimu sana. Tutumie kuhamasisha hatua katika maeneo matatu muhimu: Kutokomeza ubaguzi wa rangi wa kimfumo. Kuhakikisha haki ya fidia. Na kuharakisha maendeleo jumuishi, kwa kuhakikisha upatikanaji sawa wa elimu, afya, ajira, makazi, na mazingira salama.”
Akitambua kuwa baadhi ya mataifa yameanza kuomba msamaha kwa nafasi yao ya kihistoria katika utumwa, Katibu Mkuu ametoa wito wa “hatua za ujasiri zaidi” kutoka kwa serikali nyingi zaidi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuziwezesha nchi za Afrika, akitaka kuheshimiwa kwa umiliki wao wa rasilimali za asili na uwakilishi mkubwa zaidi katika taasisi za kifedha za kimataifa na vyombo vya kufanya maamuzi.
Mizimu ya waathiriwa wa utumwa inasubiri neno ‘haki’
Mshairi na mshindi wa tuzo kutoka Barbados Esther Phillips, ametumia mashairi mawili moja Babu zangu walinizawadia ukimya wao kuelezea jinsi mizimu ya mababu walioteswa utumwani ikitazama kizazi cha sasa huku ikikumbuka yaliyowasibu, na lingine Penzi Chungu linaloonesha hofu ya mama juu mwanae wa kiume aliyejifungua kuwa anaweza kuuzwa utumwani wakati wowote.
Akatamatisha akisema, “Mizimu ya waathiriwa wa utumwa iliyomo katika chumba hiki kwa wakati huu inasikiliza neno moja tu: HAKI. Kwa ajili yao na kwa dunia, hakuwezi kuwa na amani bila haki; haki ya fidia. Na wito huo hujibiwa tu pale maneno yanapogeuzwa kuwa vitendo! Swali Je Utafanya nini? Asanteni!”
‘Kudai kalamu yetu’
Kama ilivyo ada katika tukio la kumbukizi ya siku hii, mwakilishi wa vijana huhutubia washiriki ambapo hii leo Shahaddah Jack, ambaye ni Mshindi wa Kwanza wa Tuzo ya ushairi kutoka Toronto nchini Canada alipata fursa hiyo na kughani shairi lake liitwalo Kudai Kalamu Yetu.
Katika shairi hili anamulika vile ambavyo historia imeficha ukweli kuhusu simulizi za wale waliouzwa utumwani pamoja na kule walikotoka.
Anamulika mazuri yaliyokuweko kabla ya utumwa, ikiwemo kuvaa mavazi ambayo mtu alipenda, na kuwa na jina alilopenda badala ya kuchaguliwa na mtu.
Shairi la Shahaddah – Kudai Kalamu Yetu |
| Katika umri mdogo,mama yangu alinifundisha, kwamba kuna kurasa zilizopotea katika historia ya dunia, Na zinasikika kama majina yetu, kama majina ya bibi yangu, na wanawake waliokuja kabla yake. Wanawake waliokuwa wazao wa watumwa wa Kiafrika. Kwa namna fulani damu yangu tayari ilijua hili kuwa kweli. Kumbukumbu za dunia zinaita hili biashara. Lakini mwili wangu unalikumbuka kama wizi |
Na ndio maana Shahaddah anasema, “tunachukua tena kalamu yetu na kuyaandika majina yetu yaliyosahaulika kurudi katika kurasa za historia.”