Dar es Salaam. Kati ya majina ya madansa bora nchini, Super Nyamwela limeendelea kuwa gumzo katika tasnia ya burudani. Safari ya miaka 35 ya jina hili imebeba mambo mengi ya mafanikio yaliyotokana na juhudi, nidhamu na mapenzi ya dhati katika muziki wa dansi.

Super Nyamwela ni jina la kutafutia ugali, lakini jina lake ni Hassan Mussa. Ni dansa mkongwe ambaye mafanikio yake yamekuwa mfano wa kuigwa kwa wanenguaji (madansa) wengi waliofuata baada yake na hasa chipukizi.

Mwananchi imezungumza naye  amefunguka siri ya kufika hapa huku akijivunia mafanikio yake.

CHAMWE 04

Anasema silaha kubwa ni kujituma na kufanya mazoezi bila kuchoka tangu ameanza kazi hiyo akiwa kinda.

“Kiu yangu ya mafanikio na kujituma ndizo zilizonifikisha hapa nilipo leo,” anasema Nyamwela ambaye mbali na mafanikio ya kisanii, pia anamiliki kundi lake binafsi la sanaa linaloitwa Ubuntu Traditional Dance, pamoja na kuendesha miradi ya biashara, ikiwemo maduka, magari na makazi yake binafsi.

CHAMWE 02

Dansi yamfikisha hadi Sauzi

Anasema kutokana na kazi yake hiyo amesafiri nchi mbalimbali zikiwamo Afrika Kusini, Botswana, Namibia na Liberia na kote huko alikwenda kufanya shoo zilizomwongezea mafanikio zaidi.

“Kama si sanaa hii, pengine nisingepata nafasi ya kufika nchi nyingi kiasi hiki,” anasema.

Safari ya makundi na umaarufu

Nyamwela alianza safari yake mara baada ya kumaliza elimu ya msingi, akijikita katika sanaa huku akiendelea na masomo kwa muda.

Aliwahi kuanzisha kundi la Top Family lililotamba katika ukumbi wa ‘Kwa Macheni’, kabla ya kuasisi kundi la Billbums, ambalo baadaye wasanii wake wengi walijiunga na bendi maarufu ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.

CHAMWE 03

Hana mpango wa kuacha unenguaji

Licha ya kuwa na familia na watoto wakubwa, Nyamwela hana mpango wa kuachana na sanaa ya unenguaji, akieleza ipo ndani ya damu yake.

“Sijafikiria kabisa kuacha unenguaji niliouanza tangu mwaka 1991, nataka kuweka historia,” anasema.

Uaminifu wake kwa Twanga Pepeta

Akiwa mmoja wa nguzo muhimu African Stars ‘Twanga Pepeta’, Nyamwela anasema hana mpango wa kuondoka kwenye bendi hiyo kwa sasa.

“Kwa hapa nilipofikia, sidhani kama nitaondoka Twanga Pepeta kirahisi.”

Kuhusu kurap, uimbaji na upigaji drums na tumba

Mbali na unenguaji, msanii huyo ameongeza ujuzi katika uimbaji, kurap pamoja na upigaji wa vyombo kama tumba na drum, hatua inayomfanya kuwa msanii kamili.

Anaeleza kwa sasa anaweka nguvu kubwa katika muziki wa kuimba na kurap ili kupanua wigo wake wa kisanii.

CHAMWE 01

Kundi la Ubuntu na soko la muziki wa asili

Nyamwela pia ana kundi lake la Ubuntu, ambalo bado linaendelea kufanya kazi hasa linapopata nafasi za maonesho nje ya nchi.

Anakiri soko la muziki wa asili Tanzania bado lina changamoto, lakini anaamini linaweza kulipa kwa anayelipa uzito.

“Wasanii wengi wanaukimbia muziki wa asili wakidhani haulipi, lakini mimi naamini unalipa sana,” anasema.

Kitu ambacho hawezi kusahau

Pamoja na mafanikio yake, Nyamwela anakiri kuna matukio mawili makubwa ambayo hawezi kuyasahau maishani mwake ambayo ni, kuungua kwa nyumba yake na kufiwa na mzazi mwenzie, marehemu Halima White ambaye naye alikuwa mnenguaji.

“Haya ni mambo magumu sana kuyafuta akilini,” anasema kwa huzuni.

CHAMWE 05

Shukrani kwa Asha Baraka na msimamo wake

Nyamwela anatoa shukrani za dhati kwa mmiliki wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka, pamoja na uongozi mzima wa Twanga Pepeta kwa kumuunga mkono katika safari yake ya sanaa.

“Siwezi kumsahau Dada Asha Baraka na wote walionisimamia tangu nikiwa mdogo hadi leo,” anasema.

Ushauri kwa Wasanii Chipukizi

Akimalizia, Nyamwela anatoa wito kwa wasanii wengine kujituma na kuipenda kazi yao bila kukata tamaa.

“Jithamini, jipende na fanya kazi kwa bidii, mafanikio yapo.”

Mtazamo wake kwenye tasnia

Anasema katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya burudani nchini imeendelea kukua kwa kasi, huku wasanii wengi wakipanua vipaji vyao zaidi ya eneo moja, ikiwemo kuigiza, uimbaji na biashara, anasema  yeye ni miongoni mwa wasanii wanaoendana na mabadiliko hayo, akithibitisha sanaa inaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato na mafanikio ya maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *