Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Reuben Kwagilwa, ameagiza kuvuliwa majukumu kwa mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kufuatia kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kutokuwepo kwa nyaraka muhimu zinazohusu ujenzi wa jengo la idara ya afya, mradi uliodumu kwa takribani miaka 12 bila kukamilika.
Maelekezo hayo yametolewa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Riziki Shemdoe, na kuelekezwa kwa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya mhusika.
Uamuzi huo unafuatia maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) chini ya Mwenyekiti wake, Ado Shaibu, ambayo iliitaka TAMISEMI kufanya tathmini ya kina ya mradi huo kuanzia ulipoanzishwa hadi ulipofikia, Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa nyaraka zote muhimu za utekelezaji zinapatikana na kuwawajibisha waliokiuka taratibu.
Kamati hiyo pia ilifanya ziara ya kukagua miradi mingine ya maendeleo katika Jiji la Mwanza, ikiwemo ujenzi wa nyumba ya makazi ya mkurugenzi wa halmashauri pamoja na mradi wa soko la jiji.
(Feed generated with FetchRSS)