Dar es Salaam. Jamii imetakiwa kutowashangaa wanawake wanaofanya kazi za kiume na badala yake kuwapa moyo ili kuweza kutimiza ndoto zao katika ufanyaji wa kazi hizo.

Wito huo umetolewa na Ofisa Jinsia kutoka Shirika la Babawatoto, Christine Muyango, kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake kwa sharika hilo, iliyofanyika Mburahati jijini Dar es Salaam.

Christine amesema bado jamii ina dhana potofu kuwa kuna kazi zipo kwa ajili ya wanaume, hivyo wanapomkuta jinsi ya kike inafanya huwa wakishangaa hadi muhusika kujihisi vibaya.

”Naomba jamii tuwaache vijana kuweza kufikia ndoto, tusiwe kikwazo kwao kwani hii inawarusha nyuma katika kujikwamua kiuchumi.

“Lakini pia jamii isiwe inawashangaa wanapoona watoto wa kike wanafanya kazi ambazo walidhani ni za wanaume kwa kuwa inawavunja moyo, zaidi tuwape moyo waweze kusonga mbele,”amesema  Christine

Akielezea kuhusu shirika hilo, amesema lilianzishwa mwaka 2022 na limekuwa likitoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana na kuwapa fursa vijana ya kuweza kupata elimu katika vyuo vya ufundi kupitia mradi wake wa Ahadi.

Sambamba na hilo pia limekuwa likiwapatia vifaa mbalimbali wanayoweza kuvitumia katika uzalishaji wa bidhaa wanazoweza kuziuza kwa mmojammoja au kupitia vikundi.

Christine ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi kutambua majukumu yao katika masuala ya malezi ikiwemo kuwafuatilia katika makuzi yao lakini kuwapa mahitaji mbalimbali.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa Ahadi o, Lugano Mwakatundu, amesema  tangu kuanza kwa mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Canada na Shirika la World Vision , wameweza kuwafikia vijana  zaidi ya 3000.

Kati ya vijana hao kuna ambao wapo nje ya shule  vijana 28,000 waliopo shule wenye umri kuanzia miaka 10 hadi 18  wengine 500 wakiwa wameunganishwa na vyuo na vituo vya afya.

Pia amesema wanakuja na mradi mwingine wa uwezeshaji kiuchumi vijana unaoitwa Bloom, ambapo malengo yake ni kusaidia ule a Ahadi na wanatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 2000 ambapo wataweza kufundishwa namna ya kusimamia fedha wanazozipata kupitia shughuli mbalimbali wanayoifanya.

“Hii miradi yote miwili itafanya kazi kwa pamoja ambapo huu wa Ahadi unafanya kazi kwenye stadi za maisha lakini huu wa Bloom unakwenda moja kwa moja kwenye uwezeshaji kwani kijana ukishamuwezesha kielemu inabidi aweze kufanya shughuli yoyote ya kumuingizia kipato,”amesema Mwakatundu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti vijana walionufaika na mradi huo, Ashrafu Hamad, mkazi wa Mburahati, amesema awali alikuwa kijana wa kukaa kijiweni na kujihuisha na makundi mabaya, lakini tangu alipoingia huko maisha yake yameabadilika na sasa anaweza kujitegemea.

Fatihya Musa kijana kutoka Manzese, amesema kama kijana ameweza kupata mafunzo ya kujitambua kumebadilisha mtazamo wake juu ya ujana lakini pia kupitia mafunzo ya ufundi cherehani wameweza kujikwamua kiuchumi na sasa sio tegemezi kwa wazazi

Sauda Haji mkazi wa Tabata,amesema Babawatoto imemsadia kufanikisha ndoto yake ya tangu akiwa mdogo kupenda kuwa fundi cherehani, kwani kupitia mafunzo yao hivi sasa anaweza kushona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *