Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo Alhamisi jijini New York kutathmini hali inayoendelea kuzorota Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), likitoa kipaumbele kwa shughuli za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini humo (MONUSCO).
Kikao hicho, kimefanyika wakati kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu kuongezeka kwa ghasia na hatari ya kuyumba kwa usalama wa kikanda.
Hali ya usalama katika jimbo la Kivu Kusini bado ni tete huku Ituri ikikumbwa na hali ya kutisha ya kibinadamu na kiusalama
Akilihutubia Baraza hilo, Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu, nchini DRC Vivian Hubertina Jacqueline van de Perre, ambaye kwa sasa anakaimu uongozi wa MONUSCO, amewasilisha taswira ya kutisha ya hali ya usalama, akionya kuwa bado ni tete na inazidi kuwa ngumu.
Vivian van de Perre, Naibu Mwakilishi Maalum wa Ulinzi na Uendeshaji katika mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO, akiwasilisha taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini DRC.
Mapigano yaongezeka na mbinu mpya za kivita
Bi. van de Perre ameeleza kuendelea kwa mapigano kati ya kundi la waasi la AFC/M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC), likisaidiwa na wanamgambo wa Wazalendo.
“Hali bado inatia wasiwasi,” amesema, akisisitiza kuwa “mapigano yanayoendelea yanaendelea kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.”
Ameonya pia kuhusu mabadiliko ya mbinu za vita, akitaja “kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani (droni) za mashambulizi pamoja na kuendelea kwa kuvurugwa na kupotoshwaa kwa ishara za GPS,” jambo linaloashiria hatari ya matumizi ya teknolojia ya hali ya juu vitani.
Familia za wakimbizi wa Congo zinarudi nyumbani kwao Uvira katika jimbo la Kivu Kusini DRC kupitia bandari ya Kavimvira baada ya miezi kadhaa katika kambi ya wakimbizi nchini Burundi.
Mvutano Kivu Kusini ni hatari ya mgogoro wa Kikanda
Katika jimbo la Kivu Kusini, kaimu mkuu huyo wa MONUSCO amesema mapigano mapya yameongezeka na pia kusogeza mstari wa mbele wa vita karibu na mpaka wa Burundi.
“Hali katika jimbo la Kivu Kusini bado ni tete,” amesema, akiongeza kuwa kusogea kwa maeneo ya mapigano “kunaongeza hatari ya mgogoro kusambaa kikanda.”
Hali hii imeongeza hofu kwamba mgogoro huo unaweza kuvuka mipaka ya DRC na kuathiri zaidi utulivu wa eneo la Maziwa Makuu.
Mashariki mwa DRc kunaendelea kushuhudia wimbo la machafuko kutoka kwa makundi ya waasi ikiwemo M23
Ituri hali si shwari huku raia wanateseka
Hali katika jimbo la Ituri yanyo imeelezwa kuwa “ya kutisha,” huku Bi. van de Perre akitaja vifo vingi vya raia, watu wengi kuyahama makazi yao, na mashambulizi dhidi ya miundombinu.
Ametaja pia shambulio dhidi ya msafara wa MONUSCO na kuhusisha ghasia hizo na kundi la Convention for the Popular Revolution (CRP) linaloongozwa na Thomas Lubanga, hasa katika maeneo ya Bule na Fataki.
“Hali bado ni ya kutisha,” amesisitiza, akionyesha ukubwa wa mateso ya raia na ukosefu wa usalama.
Juhudi za kidiplomasia zatoa tumaini
Licha ya hali hiyo mbaya, Bi. van de Perre alipongeza juhudi zinazoendelea za kidiplomasia zinazolenga kupunguza mvutano na kusukuma mbele mchakato wa amani.
“Juhudi za kidiplomasia za kusaidia utekelezaji wa michakato ya amani zinaendelea,” amesema.
Amesifu pia kuimarika kwa mazungumzo kati ya DRC na Rwanda, hasa kuhusu Makubaliano ya Washington.
“Ninakaribisha dhamira mpya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda ya kuendeleza Makubaliano ya Washington,” amesema, akirejelea mkutano wa Machi 17–18 mjini Washington. “Pande zote mbili zimekubaliana juu ya hatua madhubuti za kusonga mbele katika utekelezaji wa makubaliano ya amani na kupunguza mvutano uwanjani.”
Mwakilishi wa Kudumu wa Liberia Balozi Lewis G. Brown II akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wakati muhimu kwa utulivu wa Kikanda
Wakati Baraza la Usalama linaendelea kujadili, hali mashariki mwa DRC iko katika hatua nyeti. Kuongezeka kwa ghasia, kusogea kwa maeneo ya mapigano, na mahitaji makubwa ya kibinadamu vinaashiria kuwa wiki zijazo zitakuwa mtihani mkubwa kwa juhudi za kidiplomasia na ushiriki wa kimataifa katika kumaliza mgogoro huu wa muda mrefu.
Mambo muhimu ya kuzingatia
Balozi Lewis G. Brown II Mwakilishi wa Kudumu wa Liberia kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza kwa niaba ya A3 ambazoo ni nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Somalia na nchi yale Liberia amesisitiza kwamba ingawa kuna makubaliano mengi ya amani kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na eneo zima, tatizo kuu ni utekelezaji wake.
Alipendekeza kuanzishwa kwa “Mchakato wa Kihusiano wa Utekelezaji wa Amani” wa kikanda wenye viashiria vya wazi, uthibitisho wa pande tatu, muda maalumu wa utekelezaji, na madhara kwa kutofuata makubaliano, akisisitiza kwamba amani lazima itekelezwe kwa vitendo, sio tu kuafikiwa kwa makubaliano.
Alisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa ulinzi wa raia kutokana na mgogoro mkubwa wa kibinadamu, ikiwemo kufunguliwa mara moja kwa viwanja vya ndege muhimu vya Goma na Kavumu na kuhakikisha uwajibikaji kwa mashambulio dhidi ya raia na wahudumu wa misaada.
Wanawake wa Afrika Kusini wanaohudumu kwenye mpango wa MONUSCO mjini Beni, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. (kutoka Maktaba)
Jukumu na uwezo wa MONUSCO
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha jukumu na uwezo wa Ujumbe wa (MONUSCO), akionya dhidi ya kupunguza idadi ya wanajeshi bila kuzingatia masharti ya ulinzi wa raia.
Zaidi ya hayo, amebainisha umuhimu wa uwajibikaji dhidi ya kuingilia kati kwa nguvu za nje na matumizi haramu ya rasilimali, na kuhitaji uratibu bora kati ya juhudi za kidiplomasia. Kikundi cha A3 kilithibitisha tena dhamira yake ya kudumisha uhuru, kupinga usaliti, kuleta umoja, na kulinda mipaka ya DRC.