
Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Nada Al-Nashif, ameonya kuwa hali ya usalama na haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaendelea kuzorota, akisisitiza kuwa raia “hawawezi kusubiri” wakati mazungumzo ya amani yakiendelea.
Akizungumza jana Machi 26 katika Ukumbi wa Mikutano kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa za jijini Geneva, Uswisi, amewaeleza wajumbe wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu kwamba wananchi wa DRC “wamenaswa katika mtandao mzito wa migogoro” unaojumuisha makundi ya waasi, uingiliaji wa kigeni, mvutano wa kikabila na ushindani mkali wa rasilimali asilia.
Makundi yenye silaha yaendelea kusababisha vifo na ufurushaji watu
Al-Nashif ameeleza kuwa tangu Oktoba 2025 hadi Februari 2026, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imerekodi ukiukwaji 2,560 wa haki za binadamu uliowaathiri watu 6,760, wengi wao katika majimbo ya mashariki mwa DRC.
Amebainisha kuwa raia wanashambuliwa na makundi mbalimbali ya silaha, yakiwemo M23, ADF na CODECO, pamoja na kuathiriwa na mapigano kati ya makundi hayo na jeshi la serikali. “Idadi halisi ya waathiriwa huenda ni kubwa zaidi,” ameonya.
Katika kipindi hicho, zaidi ya watu 260 waliuawa na kundi la ADF, huku maelfu wakilazimika kuhama makazi yao. Al-Nashif pia ameeleza kuwa matumizi ya silaha nzito na mashambulizi ya anga, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani, yamesababisha vifo vya raia na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Amesema, “Matumizi haya ya silaha katika maeneo yenye watu wengi yanasababisha madhara makubwa kwa raia,” akitaja pia kifo cha mfanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Karine Buisset, kilichosababishwa na shambulio la droni huko Goma.
Unyanyasaji wa kingono watumika kama silaha ya vita
Akizungumzia ukiukwaji mkubwa zaidi, anafichua kuwa katika miezi mitano pekee, takriban watu 1,300 waliuawa katika mauaji ya papo kwa papo, huku karibu watu 1,500 wakitekwa nyara. Aidha, amesisitiza kuwa unyanyasaji wa kingono unaendelea kutumika kama silaha ya vita.
“Matumizi endelevu ya ukatili wa kingono kama silaha ya vita yanasababisha mateso yasiyoweza kuelezeka kwa wanawake na wasichana wa DRC,” amesema, akiongeza kuwa mamia ya waathiriwa tayari wametambuliwa.
Kauli za chuki na mvutano wa kikabila vyaongezeka
Al-Nashif pia ameonya kuhusu ongezeko la chuki na kauli za kibaguzi, pamoja na kupungua kwa nafasi ya kiraia nchini humo. Ametoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano mara moja na kuheshimu sheria za kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji.
“Amani ya kudumu haiwezekani bila haki za binadamu,” amesema, akihimiza pia jumuiya ya kimataifa kuongeza shinikizo la kidiplomasia na kutoa rasilimali zaidi kusaidia juhudi za kulinda raia na kufanikisha amani nchini DRC.