Ni kwa kuzingatia hilo shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, FAO kwa kushirikiana na serikali ya Mapinduzi, Zanzibar, kupitia eneo la Mradi wa Pamoja wa Zanzibar, ZJP linalosimamiwa na shirika hilo, wanatekeleza mafunzo ya kilimo kinachokabiliana na tabianchi ili hatimaye kilimo cha migomba kiwe na tija sio tu kwa taifa bali pia kwa wakulima, na tayari matokeo chanya yako dhahiri.
Sasa roho zetu zimetulia – Mnufaika wa mafunzo
Mafunzo yaliendeshwa kuanzia mwaka jana kupitia kile kilichoitwa Kampeni ya Kaya kwa Kaya huko Kaskazini Pemba na tayari mashamba darasa yameshamiri na ndizi zimeanza kukomaa. Nassoro Mbao Hamadi, Katibu wa kikundi cha wakulima hawa kiitwacho Tumuombe Mungu ni shuhuda wa mafanikio haya.
Bwana Hamadi anasema, “baada ya mafunzo na kupanda kwa utaalamu sasa kuna matumaini sana, hata roho zetu zimekaa tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Tofauti migomba imekuja vizuri imestawi na inaonesha matumaini kwa wengine. Jamii tubadilike ili wengine waje waangalie waige.”
Wakulima wengi sasa wanatumia mbinu bora kama kuweka matandazo kuzunguka mgomba, kuwa na nafasi sahihi ya upandaji na utunzaji wa udongo.
Mgomba unachongwa na kisha kutumbukizwa kwenye maji
Mkulima wa migomba. Mchanga Faki Hamadi ni shuhuda wa mafanikio anasema, “tulikuwa tukilima kikawaida tu, tukichimba shimo la kawaida sana na pengine nusu mita tu bila kuutengeneza kwa aina yeyote inavyopaswa.”
Sasa mashimo ya kupanda migomba yanapimwa kwa utaalamu, “Yaani shimo tunalipatia urefu wa mita moja kwenda chini na mita moja upana, halafu tunachukua mche wa mgomba sasa, lakini tunauchonga kwanza yale magamba chini, tunaondoa yote ili kuua wadudu. Kisha tunatumbukiza kwenye maji yenye moto ili kuua vimelea.
Bi Hamadi sasa ni shukrani na matarajio akisema, “tunashukuru sana kwa kutupa mafunzo hayo na tukiendelea na migomba yetu bila shaka mavuno ya ndizi yataongezeka na tutauza tupate fedha. Tutabadilisha hata matumizi ya nyumbani kutakuwa na maendeleo tofauti na zamani.”
Vikundi 30 Pemba na Unguja kupatiwa mafunzo
Mafunzo haya ya kilimo cha migomba yanalenga vikundi thelathini katika mikoa ya Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba. Sasa unajiuliza kwa nini migomba? Mohammed Mlekwa Afisa wa Wizara ya Kilimo Zanzibar anabainisha.
“Migomba ni miongoni mwa mazao ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga pamoja na mpunga na mihogo kuwa ni zao la mkakati. Yamo kwenye sera ya serikali. Migomba limo katika sera yetu na tumeona ni zao la kimkakati ambapo ni rahisi kulifanyia usarifu na ni rahisi kuuzika. Na ni zao ambalo linahitajika kwa muda wote,” amesema Bwana Mlekwa.
Ardhi tunayo, maji tunayo tutumie sasa utaalamu
Ni kwa kutambua hilo sasa mafunzo yameelekezwa kwa wakulima shehia ya Mapofu mkoani Kaskazini Pemba. Omar Ali Omar, Mkuu wa kitengo cha wakulima kisiwani Pemba akiwa na wakulima waliopatiwa mafunzo anazungumzia umuhimu wa wakulima hao kuzingatia mafunzo.
“Huu ni mradi lakini uko chini ya Serikali ya Mapinduzi. Ina maana serikali ndiyo iliyofanya mradi uje kwetu ili tujiongezee elimu ya kilimo na tuweze kufaidika zaidi,” amesema Bwana Omar.
Ili kuepuka kusambaza magonjwa, baadhi ya mizizi ya migomba huondolewa, kisha mgomba hutumbukizwa kwenye maji ya moto na ndipo unapandwa kwenye shimo.
Ameendelea kusema kuwa, “tunajua kwamba sisi Pemba ni wazalishaji wakubwa wa ndizi katika visiwa hivi viwili, lakini ndizi zetu jamani hazina ubora. Wale wenzetu wanaokuja huwa wanashangaa nini? Mbona tunasafirisha sana ndizi? Kila meli ikiondoka ina ndizi lakini hakuna ubora kwani nini? Kumbe tatizo letu sisi liko hapa katika elimu ya uzalishaji.”
Ametanabaisha kuwa pengina wanapopata elimu, hawaitumii vizuri hivyo, “niwaambieni kitu kimoja jamani katika sekta muhimu duniani hakuna kitu muhimu kama kilimo. Sasa naomba kitu kimoja elimu hii tayari mmeshapata. Ninyi wenyewe ni mashahidi kwamba unapotumia utaalamu unapata ndizi kubwa, lakini unapofanya vingine vyovyote unapata mavuno madogo. Jamani tubadilikeni. Serikali inataka tubadilike ili ifikie wakati sisi tuwe ni wazalishaji wazuri kwani ardhi tunayo, maji tunayo. Yaani tuna kila kitu ambacho Mungu katupatia.”
Kutoka hapo Kaskazini Pemba mafunzo yameelekezwa kisiwani Unguja Zanzibar.