
Zimbabwe inasema raia wake kumi na watano, wameuawa, baada ya kusajiliwa katika jeshi la Urusi kwenda kupigana nchini Ukraine, huku wengine zaidi ya 60 wamekwama katika mstari wa mbele kwenye vita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Waziri wa Habari Zhemu Soda, amethibitisha idadi hiyo akieleza kuwa raia wa Zimbabwe waliojipata kwenye vita hivyo, walidaganywa kuwa watapata ajira zenye malipo mazuri, kabla ya kujipata kwenye uwanja wa mapambano.
Aidha, ameeleza kuwa kilichofanyika ni utapeli, kutumiwa vibaya na kulanguliwa kwa raia wa Zimbabwe ambao sasa umesababisha mauaji hayo.
Serikali ya Zimbabwe inasema tayari ipo kwenye mazungumzo na serikali ya Urusi, kuhakikisha kuwa miili ya raia wa nchi wake waliouawa inarejeshwa nyumbani pamoja na wale ambao wanaendelea kupigana.
Hii ni mara ya kwanza kwa Zimbabwe, kukiri wazi kuwa raia wake wanalipigania jeshi la Urusi nchini Ukraine.
Zimbabwe inajiunga na mataifa ya Kenya, Ghana na Afrika Kusini, ambao raia wake pia wanapigania Urusi.