
Rais wa Russia amesema tathmini ya matokeo ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran inaweza kulinganishwa na matokeo mabaya ya janga la virusi vya corona, na vita hivi vimepunguza kasi ya maendeleo ya kanda na mabara yote.
Rais wa Vladimir Putin alisema hayo jana Alkhamisi katika Kongamano la 35 la Muungano wa Wafanyabiashara na Wajasiriamali wa Russia huko Moscow na kuongeza: “Leo, hali ya kutokuwa na uhakika na hata wasiwasi katika masoko ya kimataifa imeongezeka duniani kote kutokana na uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.”
Rais wa Russia ameongeza kuwa: “Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimesababisha uharibifu mkubwa kwa vifaa, uzalishaji na minyororo ya usambazaji wa kimataifa, kwani viwanda vyote vinavyohusiana na uchimbaji na usindikaji wa hidrokaboni, metali, mbolea, na bidhaa zingine nyingi vimeshambuliwa.”
Wakati huo huo, Dmitry Peskov, msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, akizungumzia matokeo ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, amesisitiza kuwa: “Vita hivi lazima vikome haraka iwezekanavyo.”