
Wakati ukikaribia kwa ajili ya kufanyika mazishi ya mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika miji ya Najaf Ashraf na Karbala Mualla, Iraq inashuhudia maandalizi makubwa yasiyokuwa ya kawaida yanayohusisha serikali, wananchi, viongozi wa makabila, vikosi vya usalama na taasisi za huduma.
Ripoti zinasema, Iraq kwa sasa inajiandaa kwa moja ya matukio makubwa zaidi ya kidini na kisiasa katika miaka ya hivi karibuni. Wakati wa kuhamishwa mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenda Iraq ukikaribia, hali ya nchi hiyo imejaa maandalizi ya kufanikisha hafla kubwa itakayofanyika kesho siku ya Jumatano katika miji ya Najaf Ashraf na Karbala Mualla.
Tayari taasisi zote za serikali, mashirika ya wananchi, makabila, vituo vya kidini na vikosi vya usalama vimewekwa katika hali ya tahadhari ili kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa mafanikio makubwa.
Kutangazwa likizo rasmi katika mikoa saba ya Iraq, kuundwa kwa kamati maalumu, kuhamasishwa kwa vikosi vya Hashd al-Shaabi, maandalizi ya mawkibu za Husseini, pamoja na utayari uliotangazwa na viongozi wa makabila na taasisi za wananchi, vinaonyesha azma kubwa ya Wairaqi ya kuandaa hafla wanayoitaja kuwa ya kihistoria, ishara ya uaminifu na utiifu wao kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi na uthibitisho wa kuendelea kushikamana na njia ya muqawama.
Vyombo vya habari vya Iraq vimeripoti kuwa katika miji ya Baghdad, Najaf, Karbala, Diwaniyah, Nasiriyah, Basra na mikoa mingine, mikutano ya uratibu na maandalizi ya kiutendaji kwa ajili ya kuupokea mwili huo inaendelea bila kukoma.
Kwa mujibu wa mtandao wa Al-Ahd, katika Uwanja wa Al-Hamza katikati ya Baghdad, shughuli kubwa zinaendelea za kuandaa maeneo yatakayotumika katika hafla hiyo pamoja na kuboresha miundombinu inayohitajika. Kamati za utekelezaji zinafanya kazi usiku na mchana kupanga namna ya kusimamia idadi kubwa ya waombolezaji wanaotarajiwa kuhudhuria.