Askari mwingine wa kulinda amani alijeruhiwa kwa kiasi kikubwa katika tukio hilo hilo.
Guterres ametuma “salamu zake za pole za dhati” kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake na askari huyo aliyeuawa, pamoja na taifa la Indonesia. Halikadhalika amemtakia ahueni ya haraka askari aliyejeruhiwa.
Ukiukwaji wa sheria ya kimataifa
“Tukio hilo ni moja ya vitisho kadhaa vya hivi karibuni dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi katika eneo hilo lenye mvutano mkubwa,” imesema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa katika saa 48 zilizopita, matukio kadhaa yameibua wasiwasi kuhusu usalama na ulinzi wa wafanyakazi wa kimataifa wanaohudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu amesisitiza tena wito wake kwa pande zote zinazohusika kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, akisisitiza “umuhimu wa kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi na mali za Umoja wa Mataifa wakati wote.”
Timu ya wauguzi wa kikosi cha walinda amani wa UN kutoka Indonesia kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa UNFIL wakienda kutoa huduma kwenye moja ya nyumba katika Kijiji cha Rabb Tlettine, Kusini mwa Lebanon. (12 Oktoba 2012)
Ameonya kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ni kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701, na yanaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
“Uwajibikaji lazima uwepo,” taarifa hiyo imesisitiza.
Heko watendaji mnaofanya kazi katika mazingira magumu
Guterres pia amewapongeza wanaume na wanawake wanaohudumu UNIFIL, akibainisha umuhimu wa kazi yao na kusisitiza haja ya kuhakikisha uhuru wao wa kusafiri na usalama wa shughuli zao.
Umoja wa Mataifa umerejelea tena wito wa kupunguza mvutano mara moja kati ya pande husika na kuhimiza utekelezaji kamili wa masharti ya Azimio 1701, ambalo limeongoza makubaliano tete ya usitishaji wa mapigano kati ya Israel na Hezbollah tangu mwaka 2006.
UNIFIL, iliyoanzishwa kusimamia usitishaji wa uhasama na utulivu kusini mwa Lebanon, inaendelea kufanya kazi katika mazingira yanayozidi kuwa magumu huku mvutano ukiendelea katika eneo hilo.