MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema kuwa mwenendo wa hati za ukaguzi kwa mashirika na taasisi za serikali umeendelea kuimarika, ambapo hati 1,326 kati ya 1,339 zimeridhisha.
Kichere ametoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam, wakati akiwasilisha ripoti za CAG kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Ameeleza kuwa matokeo ya ukaguzi yanaonesha asilimia 99 ya hati zote ni za kuridhisha, huku hati 10 zikiwa na mashaka na hati moja ikiwa mbaya.
“Kati ya hati 1,339 zilizokaguliwa, hati 1,326 sawa na asilimia 99 zimeridhisha, hati zenye mashaka ni 10 sawa na asilimia 0.8, na hati mbaya ni moja sawa na asilimia 0.1. Aidha, taasisi mbili zimeshindwa kutoa maoni ya ukaguzi,” alisema Kichere. Ameongeza kuwa kwa ujumla, hali hiyo inaonesha kuwa utayarishaji wa hesabu katika taasisi nyingi unazingatia kanuni na viwango vinavyotakiwa. SOMA: Samia: Tudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma
Kuhusu utendaji wa kifedha wa mashirika ya kibiashara, amesema kumekuwa na upungufu wa hasara kutoka shilingi bilioni 412.3 hadi bilioni 307.7. Alifafanua kuwa kupungua huko kunatokana na ruzuku za matumizi ya kawaida pamoja na gharama za mishahara zenye thamani ya shilingi bilioni 105.2.
Aidha, amesema bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 imefikia shilingi trilioni 50.2, ambapo mapato ya ndani yalichangia shilingi trilioni 47, sawa na asilimia 93.1.Amepongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. “Mapato ya ndani yamefikia asilimia 99.4 ya lengo, jambo linaloonesha utendaji mzuri wa TRA uliovuka malengo,” alisema.
Kwa upande wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ripoti imebaini kuwa waajiri hawajawasilisha michango yenye thamani ya shilingi trilioni 2.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 85. Amependekeza mifuko hiyo iingie mikataba rasmi ya malipo na waajiri ili kuimarisha ufuatiliaji na kuhakikisha madeni yanakusanywa kwa wakati.
Amesema Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unadai takribani shilingi trilioni mbili, ambapo shilingi bilioni 562 zimepitiliza zaidi ya miezi 12 bila kulipwa. Aidha, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unadai shilingi bilioni 89.8, huku madeni mengi yakihusisha taasisi chache. Hatahivyo amezitaka taasisi za umma kuzingatia sheria za manunuzi ya umma na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
