Ugomvi nyumbani, ugoni vyaongoza mauaji 2025Ugomvi nyumbani, ugoni vyaongoza mauaji 2025

MIKOA ya Kagera, Singida na Dodoma imeibuka vinara wa matukio ya mauaji nchini kwa mwaka 2025, kwa mujibu wa takwimu mpya za Jeshi la Polisi. Ripoti ya Hali ya Uhalifu na Usalama Barabarani inaon esha kuwa jumla ya matukio 1,921 ya mauaji yaliripotiwa kati ya Januari na Desemba 2025. Idadi hii imepungua kwa matukio 272, sawa na asilimia 12.4, ikilinganishwa na matukio 2,193 ya mwaka 2024.

Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Ramadhani Kingai, amesema kuwa taarifa hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wadau mbalimbali wa usalama. Kwa mujibu wa takwimu hizo, Kagera iliongoza kwa matukio 122 ya mauaji, ikifuatiwa na Singida (98) na Dodoma (97), huku Iringa na Mwanza zikirekodi matukio 92 kila moja.

Katika kipindi hicho, watu 1,977 walipoteza maisha, ambapo wanaume walikuwa 1,502 na wanawake 475. Sababu kuu zilizochangia mauaji hayo ni migogoro ya kifamilia iliyosababisha vifo 395, ikifuatiwa na wivu wa kimapenzi (330) na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi (321).

Sababu nyingine ni pamoja na imani za kishirikina, ugomvi vilabuni, migogoro ya ardhi, visasi na kugombea mali. Aidha, vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi vilipungua, ambapo watu 321 waliuawa mwaka 2025 ikilinganishwa na 405 mwaka 2024. SOMA: Wivu wa mapenzi wapelekea mauaji Igunga

Kwa upande wa migogoro ya ardhi, jumla ya kesi 1,721 ziliripotiwa na kusababisha vifo vya watu 98, majeruhi 118 pamoja na uharibifu wa mali ikiwemo mashamba na mifugo. Wakati huohuo, Jeshi la Polisi liliripoti kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa, ambapo mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita iliongoza.

Wahamiaji wengi walitoka nchi za Burundi, Rwanda, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Kenya.Kwa jumla, kesi 1,082 zinazohusiana na uhamiaji haramu zilifunguliwa, zikiwahusisha watuhumiwa 3,334.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *