
Keir Starmer, Waziri Mkuu wa Uingereza, amesisitiza tena msimamo wa London kuhusu vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, na kusema kuwa vita hivi sio vya Uingereza na kwamba nchi yake haitaburuzwa kuingia kwenye vita hivyo.
Keir Starmer alisema siku ya Jumatatu, akizungumzia wasiwasi wa umma kuhusu kuongezeka vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kwamba ni jambo la kawaida kwa Waingereza kuwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mgogoro huo wanaposikia habari za vita. Amesisistiza: “Kwa hivyo, ni muhimu sana nikariri msimamo wangu na ule wa serikali ya London, kwa sababu vita hivi sio vita vyetu na hatutaburuzwa kuviingia.”
Tangu kuanza vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, Waziri Mkuu wa Uingereza amekuwa akitilia shaka msingi wake wa kisheria na kutangaza kuwa nchi yake haitashiriki katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, alikubali Marekani itumie vituo vya kijeshi vya Uingereza katika eneo, jambo ambalo limekabiliwa na wimbi la upinzani wa ndani na wa umma.
Katika upande wa pili Ujerumani imesema kwamba vita vya Marekani na Israel katika Asia Magharibi vitatoa changamoto kubwa kwa uchumi wa Ulaya
Wakati huo huo, Friedrich Mertz Kansela wa Ujerumani ametoa tena wito wa kusitishwa mara moja uvamizi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, akionya kwamba vita vinaweza kuleta matatizo makubwa katika uchumi wa Ulaya. Akizungumza na waandishi habari Jumatatu mjini Berlin, Mertz amesema suala la nyuklia na shughuli za kikanda za Iran “haziwezi kutatuliwa tu kwa njia za kijeshi.”