Kibaha. Abiria kadhaa waliokuwa wakisafiri na basi la Kampuni ya Katarama kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza wamenusurika baada ya basi hilo kupinduka wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano, Aprili 1, 2026, ambapo baadhi ya abiria walieleza kuwa ajali ilitokea baada ya dereva kuamua kutumia barabara ya mchepuko kukwepa foleni.

“Tulitoka Dar es Salaam jioni kuelekea Mwanza. Tulipofika Kibaha kulikuwa na foleni kubwa, hivyo dereva akaamua kupita barabara ya mchepuko. Akiwa anaendelea na njia hiyo, basi likapinduka, lakini hakuna aliyepoteza maisha,” amesema mmoja wa abiria, Lazaro Komba.

Baadhi ya wanachi wakiwa eneo kulikotokea ajali ya basi hilo. Picha na Sanjito Msafiri

Ameongeza kuwa wakati wa ajali, basi halikuwa katika mwendo kasi.

Abiria mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema wameokoka kwa bahati, lakini wana wasiwasi kuhusu hatima ya safari yao huku giza likianza kuingia.

“Tunamshukuru Mungu kwa kutuokoa. Hata hivyo, hatujui tutafikaje tulikokuwa tunaelekea. Tunaomba kampuni itupatie usafiri mwingine ili kuendelea na safari,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salum Mokase, amesema yuko njiani kuelekea eneo la tukio kwa ajili ya kupata taarifa zaidi.

Hakuna taarifa ya vifo iliyothibitishwa hadi sasa, huku uchunguzi wa chanzo cha ajali ukiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *