.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Tunaanza uchambuzi wetu na gazeti la the Financial Times na habari yenye mada “Iran huenda ikaibuka kuwa na nguvu na ikawa hatari zaidi baada ya vita hivi”

Uchambuzi huo unasema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump “amekuwa akitumia ujuzi kushinikiza adui wake kutumia nguvu walizonazo” na kuongezea kuwa vita vya kibiashara na China viliisha wakati Beijing ilizuia uuzaji wa madini yake adimu, na kuchochea Washington kupunguza ushuru waliowaekea.

Kulingana na uchambuzi huo wa Financial Times, njia sawia inatumika Iran, kuonyesha ubabe wake kupitia mlango wa bahari wa Hormuz kwa kutishia kuifunga.

Iran inatumia mlango wa bahari wa Hormuz kwa manufaa yake ili kuibuka na nguvu katika jukwaa la kimataifa baada ya vita kuisha.

Iran pia imeweza kusababisha uharibifu katika mataifa ya Ghuba kama vile Saudi Arabia na Falme za Kiarabu na kuhatarisha usalama wa mataifa haya.

Huenda Iran ikapata kipato zaidi kwa kutoza ada za ziada meli zinazopitia mlango wa bahari wa Hormuz.

Kwa kawaida zaidi ya meli 140 hupitia mlango huo wa bahari, na iwapo meli hizo zitatozwa ada zaidi, basi itaipa Iran faida ya mabilioni ya fedha.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amekosoa vikali ada zaidi inayotozwa meli zinazopita eneo hilo akisema ni kinyume cha sheria na haikubaliki.

Lakini njia mbadala ni ipi?

Uchambuzi huo unasema hakuna njia sahihi haswa, na kuwatuma wanajeshi wa Marekani kukiteka kisiwa cha Kharg hakutasuluhisha changamoto hiyo.

Wataalam wa masuala ya kijeshi wanasema jiografia ya eneo hilo la Hormuz, inaifanya kuwa vigumu kukidhibiti kikamilifu, haswa ukizingatia uwezo wa kijeshi wa Iran.

“Vita ambavyo havikufaa kuanza”

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Gazeti la Uingereza la The Guardian lilichapisha uchambuzi wenye mada “Vita vya Trump nchini Iran.”

Gazeti hilo linasema kuendelea kwa vita vya Iran kwa wiki ya tano kunaonyesha kwamba vita hivyo vilianza bila mkakati wa kina.

Uchambuzi huo unasema kuwa semi za kukinzana kutoka kwa Rais Trump zimekuwa nyingi mno, na haziwezi kuficha upungufu wa mafuta na bidhaa unaoshuhudiwa duniani.

Hali hii ina uwezekano mkubwa wa kuwa mbaya zaidi, ikizingatiwa kutokuwepo kwa dalili zozote za ushindi wa haraka wa Marekani au,kuanguka kwa Iran.

Gazeti la The Guardian linaelezea hali hiyo kuwa inafanana zaidi na “vita vya kuchoshana,” ambapo kila upande unatangaza mafanikio yake na kupuuza kushindwa kwake, huku ukisisitiza makosa ya mpinzani wake.

Gazeti hilo linaeleza kuwa vita hivyo havikupaswa kuanza kabisa, kwa kuwa tishio halikuwa la dharura na malengo hayakufafanuliwa wazi, jambo linalodhoofisha uhalali wake.

Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, wanabeba jukumu la kuanzisha mgogoro huo.

Gazeti hilo linasema njia bora zaidi ya kutatua vita hivyo ni kufanya mazungumzo bila masharti ya awali.

Inaeleza kuwa Donald Trump anachanganya vitisho vya kuongeza mvutano na mazungumzo kuhusu maendeleo ya majadiliano, bila dalili zozote za wazi za njia halisi ya kidiplomasia, wakati ambapo uimarishaji wa nguvu za kijeshi unaendelea.

Anaongeza kuwa Washington inalenga kubadilisha asili ya utawala wa Iran, huku Tehran ikisisitiza kukubaliwa kama ilivyo, hali inayoonyesha tofauti kubwa ambayo ni vigumu kuiziba.

Kwa mujibu wa wachambuzi, Marekani imekuwa ikiona mabadiliko ya utawala kama sehemu ya malengo yake ya kimkakati, wakati Iran inaona mashinikizo hayo kama jaribio la kuingilia mamlaka yake na hivyo kuyapinga vikali

Katika muktadha unaohusiana, gazeti hilo linaamini kuwa mgogoro na Iran hauwezi kutenganishwa na vita vya Gaza, likibainisha kuwa kukosekana kwa suluhisho huko kunatoa kwa Iran na washirika wake simulizi la “mapambano ya upinzani.”

Anaeleza kuwa hali ya Gaza haihalalishi vitendo vya Tehran, lakini inaeleza kwa kiasi fulani mwenendo wake.

Pia anamkosoa Donald Trump kwa msimamo wake wa kuiunga mkono Israel licha ya kile anachokiita “uhalifu wa kivita” katika maeneo ya Wapalestina, Lebanon na Iran, akisema kuwa hali hiyo inadhoofisha uwezekano wa kupata suluhisho la kidiplomasia.

Anahitimisha kuwa njia yoyote ya kupunguza mvutano na Iran huenda isianzie Tehran pekee, bali pia ipitie Gaza.

.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Tunamalizia ziara yetu kwa makala katika gazeti la The Wall Street Journal yenye kichwa “Dunia inahitaji Umoja wa Mataifa wenye nguvu zaidi,” iliyoandikwa na Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva.

Mwandishi anasema kuwa kila uvunjaji wa sheria za kimataifa husababisha uvunjaji mwingine, akitaja mfululizo wa migogoro kuanzia Afghanistan hadi Gaza, kupitia Iraq, Libya, Syria, Iran na Venezuela.

Anasema kwamba mpaka kati ya kile kinachoruhusiwa na kile kilichokatazwa unazidi kufifia polepole, kutokana na kile anachokiita “ukimya wa ushirika” wa UN Security Council.

Anabainisha kuwa matumizi ya kura ya turufu (veto) na wanachama wa kudumu yamegeuka kuwa chombo kinachotumika kama “kinga na silaha” nje ya roho ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, jambo linaloweka hatima ya mamilioni ya watu hatarini.

Anaongeza kuwa hadi hivi karibuni, nchi zilikuwa zinatafuta uhalali wa kisheria kupitia Umoja wa Mataifa, lakini hali hiyo haipo tena, kwani neno la mwisho sasa linaamuliwa na matumizi ya nguvu.

Anasisitiza kuwa sheria zilizowekwa na mashirika ya kimataifa hazina tena uwezo wa kuzizuia nchi zenye nguvu, akionya kuhusu kuongezeka kwa hali ya kutokuwepo kwa usalama kutokana na kukosekana kwa mchango madhubuti wa taasisi hizo.

Anaonya kuwa “vurugu hutawala pale ambapo hakuna vizuizi katika matumizi ya nguvu,” akibainisha kuwa dunia kwa sasa inashuhudia migogoro ya kijeshi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *